DODOMA KUFUNGUA MAKTABA KILA WILAYA


Mkutubi wa maktaba ya Mkoa wa Dodoma, Judith Lugongo

📌NA RACHEL CHIBWETE

MKUTUBI wa maktaba ya Mkoa wa Dodoma, Judith Lugongo amesema kuwa wana mpango wa kufungua maktaba kila Wilaya ili kuwawezesha wananchi wa vijijini kusoma vitabu badala ya kusafiri hadi mjini Dodoma.

Lugongo ametoa kauli  hiyo wakati  akizungumza na CPC blog kuhusu usomaji wa vitabu kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma baada ya shule na vyuo kufunguliwa nchini.

Amesema usomaji wa vitabu katika maktaba ya mkoa bado ni wa kusua sua kutokana na wanafunzi ambao ni wateja wao wakubwa kutumia muda mwingi wakiwa shuleni tofauti na siku za nyuma.

Amesema ili kuboresha usomaji wa vitabu kwa wananchi maktaba hiyo ina mapango wa kufungua maktaba kwa kila wilaya kwani mpaka sasa ni wilaya moja tu ya Kongwa ndiyo ina maktaba huku wilaya nyingine zikiwa hazina.
Tuna mpango wa kufungua maktaba kila Wilaya ili kuwawezesha wananchi wanaoishi vijijini kujisomea vitabu huko badala ya kusafiri mpaka huku mjini kwa ajili ya kujisomea au kuazima vitabu
Judith Lugongo


“Tumeshafungua maktaba moja Wilaya ya Kongwa ambapo mpaka sasa wananchi wa Wilaya hiyo wanaitumia maktaba hiyo kujisomea vitabu bure bila kulipia gharama zozote za mwaka na kuna wateja wengi wanaokwenda kujisomea hapo,” amesema Lugongo.

Amesema nguvu kubwa hivi sasa inalekezwa kwenye Wilaya zingine ambapo kuna majadiliano yanaendelea na ofisi za wakuu wa Wilaya husika ili waweze kupeleka huduma za maktaba kwa wananchi.

Amesema gharama za kusoma kwenye maktaba ya mkoa kwa mwaka siyo kubwa ni rahisi ambapo kila mwananchi hata mwenye kipato cha chini anaweza kumudu ada yake.

Mmoja wa wasomaji katika maktaba hiyo Dk Erasto Kano aliwataka wananchi wasiogope kwenda kusoma kwenye maktaba ya mkoa kwa kuwa ni ya umma.

Amesema nje ya kuwa na vitabu vya masomo mbalimbali yanayofundishwa shuleni lakini pia kuna vitabu vya hadithi, vitabu vya ujasiriamali, kilimo  na ufugaji pamoja na magazeti ya kila siku ambayo yanasomwa na watu wazima pia.

Naye Agnes Kalumuna amewata wanafunzi waliopo vyuoni kuitumia maktaba ya mkoa kwa kuwa kuna vitabu ambavyo haviko kwenye maktaba za vyuoni lakini wakija maktaba ya mkoa wanavikuta.


Post a Comment

0 Comments