WASICHANA KUNDI HATARI KWA UKIMWI

Baadhi ya maaskofu wa makanisa ya Pentecoste nchini wakiwa kwenye
semina na kupambana na Ukimwi jijni Dodoma


📌NA RACHEL CHIBWETE

KUNDI la vijana wa kike limetajwa kuwa hatari katika mambukizi ya Ukimwi kuliko vijana wa kiume na takwimu zinaonyesha kwa ujumla wao asilimia 40 ya vijana nchini Tanzania wanaishi na maambukizi ya ugonjwa huo.

Inaelezwa kuwa, asilimia 80 ni vijana hao ni wakike huku maambukizi mapya kwa siku nchini yakikadiriwa kuwa yanafikia watu 200.

Takwimu hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na mratibu wa mwitikio wa viongozi wa dini, Jovin Riziki wakati akizungumza na maaskofu wa makanisa ya Pentecoste nchini akiutambulisha mradi wa Hebu Tuyajenge.

Mradi huo unaotekelezwa na Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi Tanzania (NACOPHA) kwa ufadhili wa serikali ya Marekani (USAID) kupitia Mfuko wa dharura wa kupambana na ukimwi (PEPFAR).
Jovin Riziki akifafanua jambo kwa Mwandishi Rachel Chibwete

Riziki amesema ongezeko la idadi ya watu wanaoambukizwa Ukimwi limetokana na ukimya uliopo miongoni mwa jamii kuhusu ugonjwa huo na kuwataka Watanzania kuvunja ukimya kuhusu Ukimwi.
Amesema idadi ya maambukizi mapya kwa siku kufikia watu 200 sio jambo dogo, kwani kwa inaweza kuwa watu wengi zaidi lakini wengi wao ni wanawake na vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.

Hii inatokana na ndoa za utotoni kwa vijana wa umri huo wanaolewa na watu wazima ambao hawajui historia yao ya maambukizi na hivyo kujikuta wameshaambukizwa ukimwi katika umri mdogo
Jovin Riziki

Ameutaja Mkoa wa Dodoma kuwa upo kwenye idadi ya mikoa inayoozesha wasichana katika umri mdogo kwani asilimia 55 ya wasichana mkoani humo huolewa wakiwa chini ya miaka 18.

Mratibu huyo amewataka viongozi wa dini kuvunja ukimya uliopo katika kuzungumzia ugonjwa wa Ukimwi na kuwataka wapaze sauti zao katika kuwahamasisha watu kupima na kujua hali zao ili waweze kutumia dawa kwa watakaokutwa na maambukizi.

Amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kukutana na watu wengi mara kwa mara hivyo ni rahisi kuwahimiza kwenda kupima afya zao na kujua kama wana maambukizi na wale watakaokutwa na maambukizi waanze kutumia dawa bila kuacha.

Mratibu wa mwitikio wa viongozi wa dini kwenye mapambano ya Ukimwi Jovin Riziki
akizungumzia mradi wa Hebu Tuyajenge kwa maaskofu wa makanisa ya Pentecoste
Tanzania Jijini Dodoma

Mwenyekiti wa makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Askofu Peter Konki, amesema umefika wakati kwa viongozi wa dini kupaza sauti zao kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kama ilivyokuwa kwenye ugonjwa wa Corona.

Askofu Konki amesema ni wajibu wao kupinga unyanyapaa na unyanyasaji kwa watu wanaoishi na Virus Vya Ukimwi ili kuhakikisha ugonjwa huo unakwisha.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa kanisa la Pentecote Assemblies of God (PAG) Dk Daniel Awet, amesema ni wajibu wa viongozi wa dini kuhakikisha kuwa watu wanakuwa na afya njema hivyo watahamashisha waumini wao kupima na kutumia dawa za kufubaza makali ya ukimwi kama inavyotakiwa.

Askofu Awet ameahidi kwamba kanisa litaanza kuwahamasisha walioacha kutumia dawa ili waanze kutumia kwa faida ya afya zao.

Post a Comment

0 Comments