"HOTELI NYINGI HAZINA HADHI" KANYASU AWATAKA WAWEKEZAJI HOTELI DODOMA


SERIKALI imewataka Wawekezaji nchini kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Hoteli zenye hadhi ya nyota nne hadi tano jijini Dodoma. Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu katika hafla ya kutoa daraja za nyota kwa hoteli zilizopangwa katika daraja za ubora Jijini Dodoma.

 Kanyasu amesema licha ya Jiji la Dodoma kuwa ndio makao makuu ya Serikali lakini bado kuna mahitaji ya hoteli zenye hadhi ya nyota nne na tano hivyo akawataka wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo kwa kujenga hoteli zenye ubora.

 “Wito wangu hatuna hoteli zenye nyota nne na tano hapa Dodoma,niwaombe wawekezaji kuchangamkia fursa hii,kutafuta maeneo kwani Jiji la Dodoma linatoa na maeneo hayo yapo,”

 Amesema kuwepo kwa hoteli nzuri kutachangia kuwafanya watalii ambao huja nchini kufikia katika maeneo yenye ubora hivyo kuliongezea Taifa mapato.

 “Hitaji la wageni ni malazi na huduma bora hivyo upangaji wa madaraja ni jambo muhimu ,wito wangu kwa wamiliki wa hoteli kuwa na lugha nzuri kwa wageni ambao wanawapokea,”amesema.

 Aidha,amesema changamoto ambazo wamekuwa wakikutana nazo ni hoteli kujengwa sehemu ambazo sio sahihi pamoja na kuwepo kwa wafanyakazi ambao hawana sifa.

 “Niwaombe wamiliki wa hoteli ambazo tumezikagua na kukuta hazijakidhi vigezo kuliangalia kwa umakini jambo hili kwa kujenga sehemu sahihi pamoja na kuchagua wafanyakazi wenye sifa,”amesema.

Hoteli zilizopandishwa hadhi jijini Dodoma na kuwekwa kwenye ubora wa nyota tatu ni Fantacy Village,Nashera Hoteli na New Dodoma Hoteli.

 Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Profesa Adolf Mkenda amesema zoezi la kupanga madaraja ya nyota kwa holeli lilianza katika Mikoa ya Dar es salaa,Pwani,Arusha,Mara na sasa Dodoma.

 Amesema lengo la zoezi hilo ni kubaini ubora wa hoteli ili kuwasaidia watanzania pamoja na wageni ambao wanatoka nje ya Tanzania kujua ni sehemu gani wanatakiwa kufikia pindi wanapokuja nchini na kujua ubora wa hoteli.

 Amesema wameanzisha Mfumo wa Kieletroniki ambao utakuwa ukiwawezesha wamiliki wa hoteli kupima ubora wa hoteli zao. Katibu Mkuu huyo alisema kwa Mkoa wa Dodoma walikagua,hoteli,nyumba za wageni 428 ambapo walizokuta zenye ubora ni 24 pekee.

Post a Comment

0 Comments