KUELEKEA MKUTANO MKUU WA CCM: WAANDISHI DODOMA WAASWA KUFUATA MAADILI YA KAZI YAO


BAADHI ya waandishi wa habari watakaoripoti habari na matukio ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 11 hadi 12 mwezi huu, wamesema mafunzo ya namna ya kuripoti mkutano huo yamewajengea uelewa utakaowawezesha kuhabarisha umma kwa ufasaha na ueledi.
Wamesema mafunzo ya aina hiyo ni yakwanza kupewa, hivyo yamewajengea uwezo zaidi, kujiamini na kufahamu baadhi ya mambo ya msingi kuhusu mkutano huo wa ngazi ya juu wa CCM.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika jana jijini hapa katika Ofisi za Uhuru Media Group (UMG), Richard Mwaikenda, mwandishi kutoka Blogu ya CCM, alisema licha ya ukongwe wake kwenye tasnia ya habari lakini ni mara ya kwanza kupatiwa mafunzo hayo.
Wengi waandishi wa habari wanachojua ni kuandika habari, lakini kufahamu mambo ya msingi kuhusu CCM baadhi hawajua hata Ilani au Katiba ya CCM inasemaje. Kutofahamu mambo hayo kunajenga ukakasi kama mwandishi ana uwezo wa kuandika habari kuhusu CCM.
Richard Mwaikenda



Amesema waandishi wa habari wanapaswa kufahamu kusoma maandiko mbalimbali ya chama kutawajengea uwezo wa kuchambua na kuandika habari zinazohusu CCM.
Naye, mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Aboubakar Famau, amesema waandishi wa habari bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kiusalama.
Amesema mwandishi anapokwenda kuripoti habari kuhusu chama cha siasa lazima masuala ya usalama wake uzingatiwe ili aweze kutimiza majukumu yake kwa ufasaha.
Mwandishi wa habari kutoka gazeti la Nipashe, Agusta Njoji, alisema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa yatakayowawezesha kuandika habari kutoka vyanzo sahihi.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari  Mkoa wa Dodoma (CPC) Mussa Yusuph, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa mwandishi wa habari kwani kabla hajaripoti habari kuhusu tukio lolote la kisiasa, kuna mambo ya msingi anapaswa kuyazingatia.
Ameyataja mambo hayo kwanza ni lazima mwandishi afahamu kwa undani katiba, kanuni, sera na ilani ya chama husika  na mienendo na tabia za wanachama wake.

Pia mwandishi wa habari anatakiwa kufahamu mazingira ya eneo ambalo anakwenda kuchukua habari hususani usalama wa eneo, aina gani ya nguo anazopaswa kuvaa na ajizuie kuegemea upande wowote bali aripoti kwa kuzingatia msingi ya taaluma inavyomtaka.
 Mussa Yusuph

Akitoa mada kwenye mafunzo hayo yalioandaliwa na Uhuru Media Group (UMG) ikishirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (CPC), Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa UMG, Ernest Sungura, amesema kuna baadhi ya mambo ambayo waandishi wengi wamekuwa wakiyaandika kuhusiana na Mkutano Mkuu wa CCM wakiwa hawana uelewa wa kutosha.
Ni vyema tutakapoenda kuandika habari za mkutano mkuu, kuna mambo ambayo tuwe na uelewa nayo na kuwa na taarifa rasmi kutoka kwa wahusika.
Ernest Sungura

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha waandishi wa habari wanandika habari za Mkutano Mkuu huo kwa usahihi na umakini.
Mtangazaji wa kituo cha luninga cha Azam, Joyce Mwakalinga, aliishukuru UMG na CPC, kuandaa mafunzo hayo kwani kuna mengi ameyafahamu ambayo awali hakuwa na uelewa nayo.

Pia kuwafanya wajue katiba ya CCM waelewe nini maana ya Mkutano Mkuu na taratibu zake kwa uhakika na usahihi mzuri zaidi.
Joyce Mwakalinga

Mkuu wa Kanda zote kutoka UMG, Kiondo Mshana, alisema katika mkutano huo waandishi waweke uzalendo mbele.
Tusiende kuandika mkutano huu tukiwa na agenda zetu binafsi mkononi au mtu fulani tufuate maadili ya kazi zetu
Kiondo Mshana


Kwa upande wake, Mhariri wa Mitandao ya Kijamii wa UMG, Mwanzo Millinga, alisema bado waandishi wa habari wana changamoto nyingi ikiwemo usalama wa waandishi wa habari wakati wakitekeleza majukumu yao.

Post a Comment

0 Comments