KUTOKA KUTEMBEA MIGUU PEKU MPAKA KUWA RAIS…



MWEZI Novemba mwaka jana Mzee Benjamin Mkapa alitoa kitabu juu ya maisha yake, na katika aya ya mwisho ya dibajia aliandika kuwa anatumai kuwa kitabu hicho kitatoa mchango katika historia ya Tanzania na kuwatia moyo na kuwapa maarifa viongozi wa kesho wa Bara la Afrika.

Miezi minane toka atoe kitabu hicho, Mzee Mkapa ameaga dunia jijini Dar es Salaam na kuacha kitabu hicho kama kumbukumbu yake itakoyoishi milele.

Historia ya maisha yake, toka alipozaliwa mwaka 1938 na kukua katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Lupaso, mkoa wa Mtwara mpaka kuwa rais ni simulizi ya kutia moyo.

Mkapa naeleza namna ambavyo ilimlazimu kutembea kwa umbali mrefu, miguu peku chini, kutafuta elimu katika shule za Wamishenari.

Baada ya kumaliza darasa la 10, sawa na kidato cha pili kwa mfumo wa sasa, Mkapa alitaka kuwa askari. Alipoulizwa na mwalimu wake wa kizungu kuhusu kuendelea na elimu mpaka darasa la 12 na kisha Chuo Kikuu, Mkapa anakiri kwenye kitabu chake kuwa hakujua kama kulikuwa na muendelezo huo wa masomo.

Baada ya kufaulu vizuri darasa la 12, Mkapa alienda Chuo Kikuu cha Uganda ambapo mwaka 1962 alihitimu Shahada ya Kingereza. Baada ya hapo alienda Marekani na kusomea diplomasia.

Alifanya kazi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania akianza ajira kama afisa wa wizara ya mambo ya nje na baadae kuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya chama na serikali pamoja na kuwa mwandishi wa rais Nyerere.

Mkapa pia alihudumu katika nafasi ya Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Canada na Marekani. Pia alikuwa waziri wa Mambo ya Nje katika vipindi viwili tofauti katika utawala wa Nyerere na baadaye rais wa pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Mkapa aliingia madarakani mwaka 1995 baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, baada ya kuhudumu serikalini kwa miongo mitatu.

'SIKUTEGEMEA UNGEGOMBEA URAIS'



Mwaka 1995 Mkapa alijitosa kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pasi kupigiwa upatu na watu wengi.

Katika kitabu chake, Mkapa anaeleza kuwa alimfuata aliyekuwa rais mstaafu wa Tanzania na Baba wa Taifa , Mwalimu Julius Nyerere kumfahamisha juu ya azma yake ya kugombea urais na sababu zake pia.

Mkapa anaandika kuwa baada ya kumsikiliza kwa makini Mwalimu alimjibu kuwa: "…Nitakuwa muwazi kwako. Sikutegemea kuwa ungetaka kuwania urais, wazo kama hilo halikuniingia kabisa."

Lakini si hivyo tu, Nyerere alimweleza Mkapa kuwa kuna mtu mwengine ambaye ailikuwa akimfikiria kuwa angekuwa rais bora, lakini alikuwa akisita kuingia kwenye mchuano huo. "Ben, kitu pekee ninachokuahidi ni kuwa sitakuzibia njia, sitakupinga."

Mkapa alishinda uchaguzi ndani ya chama akipata ushindani mkali kutoka kwa Jakaya Kikwete (ambaye alikuja kumrithi madaraka ya urais mwaka 2005).

Alishinda uchaguzi mkuu kwa asilimia 61.8 ya kura, huku kinara wa upinzani katika uchaguzi huo akiwa Augustino Mrema akipata 27 Augustino Mrema akipata asilimia 27.7 ya kura.

Bonyeza hapa kusoma zaidi...

Post a Comment

0 Comments