NA HAMIDA RAMADHANI
NAIBU Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Willam ole Nasha
amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 serikali imetenga kiasi cha
shilingi milioni 874 kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu nchini.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na naibu waziri huyo
wakati wa hafla ya kutunuku vyeti na zawadi kwa washindi wa mashindano ya
kitaifa ya sayansi teknolojia na ubunifu (MAKISATU) 2020.
Ole Nasha amesema ili kuendeleza bidhaa ziweze kufikia
kwenye kiwango cha kuingia sokoni na kutumika na watanzania na walaji wengine
serikali haina budi kutenga kiasi hicho cha fedha.
Aidha amesema kutokaana na jitihada za serikali za kukuza na
kuwaendeleza wabunifiu wachanga nchini inakadiriwa kuwa vijana elfu 15 wamepata
ajira zisizo rasmi na vijana 600 wamepata ajira rasmi kupitia masuala ya
ubunifu sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake naibu katibu mkuu wa wizara hiyo Profesa James Mdoe
amesema MAKISATU ni moja ya mikakati ya serikali ya kuibua,kutambua na
kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania hususa ni wale wa hali
ya chini.
Nao baadhi ya wadhamini wa mashindano hayo wameishukuru serikali
kupitia kwa wizara ya elimu,sayansi na teknolojia kwa kuanzisha mashindano hayo
yenye tija katika kuiendeleza serikali ya viwanda na hivyo kuwaomba wadau
wengine kujitokeza kudhamini.
Mashindano ya makisatu yalianzishwa rasmi mwaka 2019 na wabunifu
mahiri 60 walitambuliwa ambapo wapo katika hatua mbalimbali za kuendelezwa huku
serikali kupitia wizara ya elimu ilitoa kiasi cha milion 750 kwa ajili ya
kuendeleza ubunifu na teknolojia za wabunifu hao ili ziweze kubiashararishwa na
hivyo kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
0 Comments