MKAZI WA DAR MBARONI KWA TUHUMA YA WIZI WA DAWA ZA BINADAMU



📌NA HAMIDA RAMADHANI

JESHI la polisi mkoani Dodoma limemkamata Frederick Maxmilian (38) mkazi wa Mbagala jijini Dar es salaam akiwa na shehena ya  dawa za hospitali za magonjwa ya binadamu zinazosadikiwa kuwa za wizi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa polisi mkoani humo Gilles Muroto amesema,mtuhumiwa huyo amekamatwa Julai 9,mwaka huu akiwa na shehena hiyo yenye sampuli 149 baadhi zikiwa na nembo ya Bohari ya Dawa (MSD) .

Amesema katika mahojiano na mtuhumiwa huyo imeonekana kuwa yeye siyo daktari wala mfamasia na dawa ila anashirikiana na mfamasia ambaye ni mtumishi wa Serikali (jina limehifadhiwa) huko mkoani Tabora.

Kamanda Murotto amesema uchunguzi unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

RPC Muroto akiongea na Waandishi wa Habari


Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali  ya mkoa wa Dodoma Dkt. Samuel Seseja amesema shehena hiyo ina dawa aina nane mbapo zipo zenye  nembo ya Serikali,pia zipo zenye nembo ya MSD na  nyingine hazina nembo.

Hata hivyo amesema dawa hizo hazitakiwi kuuzwa na mtu yeyote kwani kuna wazabuni wa kufanya kazi hiyo katika kila mkoa.

Uuzaji wa dawa unalindwa na sheria inayotoa namna gani dawa hizo ziweze kununuliwa na kuuzwa, hivyo hicho ni kinyume na sheria inayosimamia suala la dawa na vifaa tiba.
Dk.Seseja.

Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na watoa huduma kutojihusisha na ununuzi wa dawa kutoka kwa vyanzo ambavyo havifahamiki na kwamba  wanapaswa kununua kwenye maduka ya dawa yaliyosajiliwa na mfamasia Mkuu wa Serikali.

Pia amewataka kutojihusisha na watoa huduma wasio waaminifu wanaoitia doa Serikali inayofanya kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi.

Amesema,hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watumishi wasio waaminifu wanaofanya hujuma ya kuchukua dawa katika vituo na hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma.

Post a Comment

0 Comments