WALIMU WANAFUNZI,CWT WAPELEKA TABASAMU BUIGIRI WASIOONA



📌BEN BAGO

JAMII imetakiwa kuwakumbuka Wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi hao kumudu msomo yao.

Wakizungumza baada ya kugawa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona iliyopo Wilaya ya Chamwino,wana Jumuiya ya Walimu Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA) wamesema jamii inapaswa kukumbuka kundi hilo la wanafunzi ili waweze  kumudu masomo yao.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Gerald Kwagilwa amesema licha ya wao kupeleka vyakula na mahitaji mengine wamegundua kuwa hata idadi ya walimu katika shule haitoshelezi mahitaji.

Katika Chuo Kikuu cha Dodoma kinatoa ‘program’ ya elimu ya mahitaji maalumu lakini walimu wanamaliza na hawana ajira.

Kwagila ameiomba serikali kuajiri walimu hao ili kuziba upungufu wa walimu hao katika vituo vya wanafunzi wenye uhitaji maalum.

Naye mweka hazina wa Jumuiya hiyo Mwalimu Teddy Gilosa amesema wameamua kutoa msaada huo wa vitu mbalimbali shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya mpango wao wa kila mwaka kurudisha  tabasamu kwa jamii.

Mwalimu Teddy amesema licha ya wanachama wa jumuiya hiyo kuchangishana ili kupata pesa za kununua mahitaji hayo kwa watoto lakini Chama Cha Walimu Tanzania nacho kimewaunga mkono katika kutimiza zoezi hilo.

UDOSTA mlezi wetu ni CWT,hivyo nao wametusaidia kwa kiasi kikubwa kupata mahitaji haya ambayo leo tumewaletea watoto hawa
Mwl.Teddy Gilosa

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo,Sospeter Jonathan amewaomba wadau kuendelea kujitokeza kuwasaidia wanafunzi katika mahitaji mbalimbali ikiwemo uboreshwaji wa miundo mbinu shuleni hapo.

Mwalimu Sospeter amesema miundo mbinu iliyopo siyo rafiki kwa wanafunzi wasioona japo anasema haiwazuii wao kutotimiza majukumu yao.

Njia(barabara) wanazotumia wanafunzi wetu wasioona sio nzuri na huwa zinaharibika sana kipindi cha masika hivyo inakuwa vigumu kufika madarasani

Shule ya Msingi ya Buigiri Wasioona ina milikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Mashariki na inaendeshwa kwa ushirikiano wa Kanisa hilo na Serikali.

Post a Comment

0 Comments