MARUFUKU KUSAFIRISHA MTOTO BILA KIBALI



WAZIRI wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amepiga marufuku wazazi au walezi kusafirisha watoto kwenye vyombo mbalimbali vya usafiri bila kibali.

Simbachawene ameyasema hayo jijini Dodoma alipokuwa akifungua maadhimisho ya kitaifa kupinga biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Amesema hali ni mbaya hasa katika maeneo ya miji mikubwa ambapo biashara ya kusafirisha watu imeshamiri hasa kwa wanawake na watoto wa kike.

Simbachawene amebainisha kwamba kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi katika Wizara yake vinatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kukabiliana na biashara hiyo haramu ya kusafirisha binadamu.
Waziri huyo amesema vyombo vya ulinzi vinatakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama ilivyozoeleka bali vinatakiwa kutimiza majukumu yao kwa vitendo.

Biashara hii hata hapa tukisema tutoke twende kwenye mabasi barabarani tukafanye ukaguzi kwenye mabasi lazima tutawakuta watoto watatu hadi wanne, ambao wanasafirishwa bila wao kujua kule wanakokwenda wanakwenda kufanya nini
Waziri Simbachawene


Amesema kutokana na hali hiyo, vyombo vya ulinzi vinatakiwa kuacha kufanya kazi kwa nadharia bali viendeshe misako mikali katika magari mbalimbali ili kukomesha biashara hiyo haramu.
Vile vile, amesema pamekuwapo na watu ambao ni maarufu kwa kukusanya watoto kutoka katika mikoa mbalimbali na kwenda kuwauza kwa watu wanaohitaji wasichana wa kazi.

Amewaonya Watanzania kutotumia kigezo cha umasikini na ukosefu wa ajira nchini kama kichocheo cha kuruhusu kirahisi vijana na mabinti kwenda nje ya nchi kwa sababu ya kutafuta kazi, ambapo alisema ni vyema kutumia fursa na rasilimali zilizopo kujikwamua.

Waziri Simbachawene amesema, watoto wengi husafirishwa kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi, baada ya kufika huko wanajikuta wanaishia kutumikishwa katika biashara ya ukahaba hususani katika nchi za India, Thailand, China, Indonesia na Malasya.

Amesema kuwa, wengine wanatumikishwa kwa kazi za ndani katika nchi za Oman na baadhi ya nchi nyingine za uarabuni ikiwemo Iraq.

Pia,Simbachawene amemuagiza katibu mkuu wa Wizara yake, kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje, ili kuwabaini na kuwarejesha nchini Watanzania wote waliopo nje ya nchi ambao wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kutumikishwa.

Ameeleza kuwa, wahanga wengi wanaosafirishwa nje ya nchi wanatokea jijini Dar es Salaam, Tanga na Dodoma (Hususani Wilaya ya Kondoa) na wachache ni kutoka mikoa mingine na waathirika wakubwa ni wanawake kuanzia umri wa miaka 16 hadi 26.

Post a Comment

0 Comments