MASHIRIKA YA KIRAIA YATAKIWA KUWATAFUTIA VYANZO VYA MAPATO WENYE ULEMAVU




📌NA RACHEL CHIBWETE

SERIKALI imeyataka mashirika yanayotoa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini kutafuta vyanzo vya mapato na kuwapatia vifaa saidizi kwa watu hao kama vile viti mwendo, mafuta ya ngozi kwa watu wenye ualbino, miwani ya jua na vifaa mbalimbali vya kuwaaidia kwenye shughuli zao.

Wito huo umetolewa leo  na Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya waziri Mkuu kitengo cha watu wenye ulemavu, Philbert Kawemama kwenye mafunzo ya matumizi ya viti mwendo kwa wahudumu wa kujitolea na maofisa ustawi wa jamii yaliyotolewa na Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kati.

Kawemama amesema ni ukweli usiopingika kwamba mashirika mengi yanatoa elimu ya haki na ustawi wa watu wenye ulemavu ambalo ni jambo jema lakini aliwataka waende mbali zaidi kuhakikisha kuwa haki hizo zinapatikana kwa kuwapatia visaidizi katika shughuli zao.

“Aidha napenda kutoa wito kwa wazazi, walezi na vyama vya watu wenye ulemavu na hasa CHAWATA kuelimisha wazazi na walezi juu ya kuwafichua watoto wenye ulemavu ili kuweza kupata viti mwendo.”

“Wote tunatambua umuhimu wa viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu wa viungo kwamba vinawasaidia kuweza kufikia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, afya na michezo mbalimbali,” amesema Kawemama,

Amesema viti mwendo vitasaidia kuondoa unyanyapaa kwa watoto wenye ulemavu kwa vile watapata fursa ya kuchangamana na wenzao wasio na ulemavu wawapo shuleni na katika maeneo mbalimbali ya huduma.

Ametoa rai kwa maofisa ustawi wa jamii nchini kuhakikisha wanaimarisha huduma za kisaikolojia na kijamii kwa watu wenye ulemavu ili kuweza kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu wenyewe kwa wenyewe au jamii na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake Kaimu meneja wa World Vision Kanda ya Kati, Zacharia Shigukulu amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa wahudumu na maofisa ustawi wa jamii ambao watakwenda kuwaibua watu wenye ulemavu kwenye maeneo yao ili waweze kupatiwa viti mwendo.

Post a Comment

0 Comments