NEC KUTOA ELIMU KWA MAKUNDI MAALUM KUTAMBUA THAMANI YA KURA



📌NA RACHEL CHIBWETE
 TUME ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) imetoa vibali kwa asasi za kiraia 252 kwa ajili ya utoa elimu ya uraia Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu.

Akizungumza na CPC Blog Ofisa Habari na Elimu kwa mpiga kura kutoka NEC, Johari Mutani amesema wametoa vibali hivyo ili viweze kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania na kuwajengea uzalendo wa kushiriki zoezi la kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu.

Amesema kati ya asasi hizo za kiraia zilizopewa kibali, 245 zitatoa elimu hiyo Tanzania Bara na asasi saba zitatoa elimu Tanzania Zanzibar.

Sisi hatutoi elimu ya uraia kwa wananchi kazi yetu ni kutoa elimu ya mpiga kura ili wananchi wengi waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi kutumia haki yao ya kikatiba, na hiyo ndiyo furaha yetu.

Lakini elimu ya uraia itatolewa na asasi zilizopewa kibali kwa ajili ya kuwajengea uwezo wananchi kuwa na uzalendo na mambo mengine katika kutumikia nchi yao na tunaamini kwa elimu hiyo watajitokeza kupiga kura,Mutani
Amesema tume hiyo imeshatoa elimu kwa makundi ya wanawake, vijana wazee na watu wenye ulemavu kuhusu umuhimu wa kuchaguza viongozi watakaowaongoza kwa kutumia kura yao.

“Pia tumewafikia makundi yaliyopo pembezoni kama vile wavuvi na wafugaji wa kuhamahama ambao wote tumeweza kuwafikia na kuwaandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwani mwanzoni walikuwa wanalalamika kuwa wamesahauliwa,” amesema.

Kwa upande wake Rashid Hizza amesema mpaka sasa elimu ya mpiga kura imeshawafikia makundi mbalimbali wakiwemo, vyama vya siasa, viongozi wa dini, makundi maalum na vyombo vya habari kwa ajili ya kuhakikisha kuwa siku ya uchaguzi mkuu kila mtu mwenye sifa anashiriki uchaguzi mkuu.

Aidha amewataka wagombea wote kufuata sheria na taratibu zote zilizowekwa na tume hiyo ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi mkuu bila kuwekewa mapingamizi yatakayowaondoa kwenye uchaguzi.

Post a Comment

0 Comments