TAMWA, MASHIRIKA WATOA MAPENDEKEZO USHIRIKI WA WANAWAKE UCHAGUZI MKUU 2020


📌NA DOTTO KWILASA.

WAKATI macho na masikio ya Watanzania yakiisubiri kwa hamu Oktoba 28 ambayo ni siku ya uchaguzi mkuu nchini, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) wametoa mapendekezo kwa  vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

Uchaguzi Mkuu unafanyika wakati ambapo kati ya wagombea 16 waliochukua fomu kugombea urais, wapo wanawake wawili mpaka sasa ambao ni Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC, na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini walioteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo.

Kadhalika, wapo wanawake watano wanaowania umakamu wa Rais, katika mchakato huu wa uchaguzi.

Kutokana na hatua hiyo,TAMWA, WiLDAF  na GPF  taasisi ambazo malengo yake ni kuwepo kwa jamii yenye amani, inayoheshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia, na amani zimeona ni vyema kuikumbusha jamii, wadau wa masuala ya siasa na ya jinsia  kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

 TAMWA WiLDAF  na GPF  chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’ imeendesha midahalo mbalimbali ya wanawake kutoka  vyama vya siasa ,wakiwamo wanawake wanasiasa, viongozi wa dini na kubaini kuwa bado kuna changamoto  zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa.

Midahalo hiyo  imefanywa katika  kanda za Dodoma, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam na kuibua changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ikiwamo lugha dhalilishi  zinazowavunja moyo wanawake  wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.

Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto  ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni, na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma.

Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake
Rose Reuben, Mkurugenzi TAMWA.


Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo wa TAMWA anasema ,kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbali mbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kunadidimiza siasa kwa wanawake.

"Wajumbe wanaotegemewa kupiga kura huwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa kitu kidogo ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea,hali hii inaathiri  wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana,"anasisitiza .

Licha ya hayo anasema taasisi hizo za Kiraia zimebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.

Anaeleza Kuwa Changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.

Kulingana na Reuben,hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo na hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.

"Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono na pia tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu,"anasema Mkurugenzi huyo wa TAMWA na kuongeza;

"Tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake,"anasema.


Pamoja na Mambo mengine Mkurugenzi wa TAMWA anasema Changamoto nyingine zilizoibuliwa katika midahalo hiyo,  ni Ilani za vyama vya siasa ambazo hazitoi nafasi kwa wanawake kuwa viongozi na kupata nafasi ya kugombea katika majimbo.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa GPF , Martha Nghambi anasema Mwaka huu wanawake wengi wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na hivyo wangependa kuviomba vyama vya siasa kuhakikisha kuwa wale wanawake wenye uwezo wasimamishwe kugombea nafasi hizo .

Aisha Nghambi anashauri  vyama kuendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake ambao hawakupata nafasi mwaka huu ili waweze kusimama na kugombea chaguzi zijazo ndani ya vyama vyao, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, hawapendani badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii,

Kauli hizi za kuwa wanawake hatupendani si za kweli bali zimekuwa zikitumika katika jamii kuwagawa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi
Martha Nghambi,Mkurugenzi GPF


Kadhalika anasema kuwa wao kama wadau wa wanawake wanatarajia kuona  wadau wa siasa na  vyombo vya usalama vitazingatia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK John   Pombe Magufuli ya kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa wanawake katika uchaguzi mkuu na katika nafasi za uongozi na maamuzi.


Anna Kulaya Mkurugenzi - WILDAF anasema,ili kuwe na Maendeleo ya usawa Katika jami wagombea wote wanapaswa  kuhakikisha kuwa hawatoi kauli zozote za uvunjifu wa Amani, kuchochea vurugu, kuwagawa watu kwa dini au makabila yao au matusi na udhalilishaji wa kijinsia kwa wagombea wengine.

Anasisitiza Kuwa   Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)inapaswa  kuendelea kuhimiza uchaguzi huru, wa haki na usawa na kutengenezwa kwa mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote.

Post a Comment

0 Comments