WATANO MBARONI KWA UHUJUMU UCHUMI



📌NA HAMIDA RAMADHANI

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imewafikisha mahakamani watu watano (5) kwa makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo makosa ya matumizi mabaya ya fedha na kuisababishia Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa hasara ya zaidi ya shilingi mil.149.

Akizungumza na waandishi wa habari  Mkuu wa Takukuru mkoani hapa Sosthenes Kibwengo amesema makosa hayo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Amesema kuwa watuhumiwa hao ambao walikuwa ni watumishi wa halmashauri hiyo ni Fanuel Senge( 67),aliyekuwa Mkurugenzi  Mtendaji, Ignace Chacha(48),aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, pamoja na Joel Nskela,aliyekuwa Afisa Mipango.

Amesema kuwa watumishi hao ambao wameshitakiwa kwa matumizi mabaya ya mamlaka wameunganishwa katika shtaka la pili la kusababisha hasara na Moses Ryakitimbo(38) ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya magoma and Rykitimbo Contractors LTD,na Gerald Massawe (43)aliyekuwa Meneja mradi wa Ujenzi wa Ukumbi wa kibiashara wa wilaya ya Mpwapwa. 

Uchunguzi wa Takukuru unaonyesha kuwa watu hao septemba 12 na Desemba 2013,watumishi hao walitoa zabuni ya ujenzi wa ukumbi wa biashara yenye thamani ya sh mil 356 kwa kampuni ya Magoma and Ryakitimbo Contractor LTD bila kufuata taratibu za manunuzi ya umma kwa bodi ya zabuni.
Sosthenes Kibwengo

Kibwengo amesema uchunguzi umeonyesha Mkandarasi alilipwa jumla ya sh milion 149,833,500.

Mbali na hilo pia wamewapandisha kizimbani aliyekuwa Afisa Elimu Msingi Abubakary Adam (57) na aliyekuwa Afisa Elimu Ufundi wote wa halmashauri ya Chamwino kwa kosa la kutumia nyaraka kumdanganya muajiri kinyume na sheria.

“Watu hao wamefunguliwa mashtaka 8 ya kugushi na shtaka moja la ubadhilifu kinyume na kifungu cha sheria namba 28.
Alisema uchunguzi wa Takukuru unaonyesha Agosti na Oktoba 2015 watuhumiwa waligushi nyaraka mbalimbali na kujipatia kinyume na taratibu sh milion 3.5 ambazo walidai walizitumia kutengeneza kasiki katika shule 12 zilizopo katika halmashauri hiyo”amesema . 

Kesi hiyo itatajwa tena septemba 24 mwaka huu katika Mahakama ya hakimu mkazi Mpwapwa chini ya hakimu Nuru Nasari. 

Hata hivyo Mkuu huyo wa TAKUKURU amewakumbusha watumishi wa umma kuacha kujisahau na kuwataka kufanya kazi kwa weledi. 

Pia amesema kuwa watumishi wanapaswa kuwa makini katika utendaji wao wa kazi za kila siku. 

Amesema Takukuru inawakumbusha watumishi wa umma kwamba jinai haifi unaweza kutenda kosa leo likaja kujulikana hapo baadae. 
 
Inawezekana ukawa hukumbuki lakini uchunguzi ukifanyika unafikishwa mahakamani bila kujua,hivyo Takukuru ipo kila kona kuangalia walarushwa hivyo jamii inapasa kuwa makini katika kazi wanazofanya.
Sosthenes Kibwengo

Post a Comment

0 Comments