WATOTO 25 HUFARIKI DUNIA KUTOKANA NA WAZAZI KUTOFUATA TARATIBU ZA UNYONYESHAJI



📌NA DOTTO KWILASA

TAASISI ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) imesema kuwa kila watoto 1000 wanapozaliwa nchini ,25 Kati yao hufariki dunia kutokana na wazazi wengi kutofuata taratibu za unyonyeshaji Kutokana na kutokuwa na uelewa juu ya masuala ya lishe kwa watoto wachanga.

Kutokana na hayo wadau wanaotetea afua za lishe nchini wametakiwa kuboresha lishe za wanawake walio katika umri wa kuzaa ili kupunguza udumavu na utapiamlo wa watoto pindi wanapozaliwa.

Hayo yamebainishwa Jana jijini hapa na mkurugenzi msaidizi wa huduma za lishe wizara ya afya , Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto Grace Moshi wakati akiongea na waandishi wa habari Kuhusu namna ya kuhamasisha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani.

Moshi amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 59 ya watoto kuanzia miezi 0-6 ndio wanaonyonyeshwa maziwa ya mama kama inavyoshauriwa na wizara ya afya huku asilimia 41 ya watoto wakiwa hawanyonyehwi  kwa utaratibu unaoshauriwa hali inayosababisha watoto wengi kuwa na udumavu.

Pamoja na hayo amesema ni jukumu la kila mama  kuhakikisha ananyonyesha mtoto wake ndani ya saa moja Mara baada ya kujifungua  kwani maziwa humpatia mtoto virutubishi vyote na maji anayohitaji kwa ukuaji katika miezi 6 ya mwanzo.

Kwa upande wake Afisa lishe kutoka TFNC Valeria Millinga amezungumzia unyonyeshaji maziwa ya mama kuwa  ni msingi wa maisha ya mtoto kwani yana asilimia 88  ya  virutubisho na viini lishe hali inayoyatofautisha na maziwa ya mengine.

Maziwa ya ng'ombe ni kwa ajili ya ng'ombe hivyo hatupaswi kuwapa watoto maziwa haya labda pale tu inapobidi na kwa kufuata ushauri na maelekezo kutoka kwa wahudumu wa afya
Valeria Millinga


Lazima kina mama wajawazito watambue faida ya unyonyeshaji maziwa ya mama kuwa kwa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama itamsaidia mtoto kuondoa uchafu wa mwanzo wa kijani  tumboni.

Aidha akieleza zaidi ametaja baadhi ya faida nyingine  ya unyonyeshaji kuwa unasaidia kumwepusha mtoto na magonjwa nyemelezi kama vile kuhara pamoja na mzio.

Pamoja na mambo mengine amewataka wanawake kuepuka kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya kopo kwani hayana virutubishi katika ukuaji wa mtoto na kusisitiza kuwa kunyonyesha huleta mahusiano mazuri na ukaribu kati ya mama na mtoto.


Naye Neema Joshua mtaalamu wa masuala ya lishe (TFNC)alisema kuwa maziwa ya mama ni chakula na kinywaji pekee kinachotosheleza mahitaji ya mtoto kwa wakati.

Licha ya hayo amebainisha mambo muhimu yanayofanikisha unyonyeshaji wa mtoto kuwa ni pamoja na kumpa mtoto vyakula vya nyongeza anapotimiza umri wa miezi 6 .

Pia amesema ili kuboresha afya ya mama na mtoto ni sharti mama akamue maziwa kwa ajili ya mtoto pindi mama anapokuwa amekwenda kufanya kazi mbali na nyumbani..

Kwa wale wazazi ambao ni waajiriwa wanaweza kukamua maziwa yao na kuyahifadhi kwenye jokofu ambapo yanaweza kustahimili kukaa kwa saa 72 ndipo yanaweza kuharibika na kwa wale ambao hawana majokofu wanaweza kukamua na kuyahifadhi sehemu salama ambapo yanaweza kukaa kwa SAA 6 hadi SAA 7 ndio yaharibike.

Wiki ya unyonyeshaji ilianza kuadhimishwa mwaka 1992 ambapo kila ifikapo tarehe mosi mwezi wa nane Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha na tamati yake ni tarehe nane mwezi wa nane ya kila mwaka ambapo kila mkoa huadhimisha kwa aina yake.

Kwa mwaka huu kauli mbiu ya wiki ya unyonyeshaji duniani inasema Tuwawezeshe  wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira,hii inatoa picha kwa jamii juu ya uhusiano huo,changamoto na suluhisho lake.

Post a Comment

0 Comments