ZUNGU AAMURU MSAKO VIWANDA VYA NONDO VINAVYOTUMIA KUNI




📌NA RACHEL CHIBWETE

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Zungu ameliagiza Baraza la usimamizi wa mazingira nchini (NEMC) kufanya msako na kuvichukulia hatua za kisheria viwanda vyote vya nondo na chuma vinavyotumia kuni kwenye shughuli zao.

Zungu alitoa agizo hilo  Jijini Dodoma alipotembelea maonyesho ya nanenane kanda ya Kati yanayofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni.

Amesema agizo hilo ni kwa nchi nzima ili kunusuru mazingira ambayo yanaharibiwa kutokana na kukata miti inayotumika kwenye kuyeyushia nondo na vyuma hivyo.

"Hivi sasa kuna nishati mbadala ambazo zinaweza kutumika kuyeyushia nondo na vyuma hivyo badàla ya kutumia kuni ambazo zinasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira."

Hapa naona kuna mkaa mweupe na mkaa mbadala ambao ni rafiki kwa mazingira na inapatikana kwa gharama nafuu kuliko kuendelea kutumia kuni kwenye shughuli za kuyeyushia chuma na nondo.
Zungu.

Amesema agizo hilo ni kwa mameneja wa NEMC kanda zote  na nchi nzima ambapo kuna viwanda vya kuzalisha chuma na nondo.

Kwa upande wake meneja wa NEMC kanda ya kati, Novatus Mushi alisema baraza hilo limekuwa likitoa elimu kwa wawekezaji kabla ya kutoa leseni ya kuwekeza nchini matumizi ya nishati mbadala ili kutunza mazingira.

Amesema elimu hiyo inatolewa ili wawekezaji wajue umuhimu wa kutunza mazingira kwenye uwekezaji wao na hata kwenye shughuli zao kwa kuwa ndiyo kipaumbele cha kwanza katika kuwekeza.

Kwa upande wake meneja wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC) kanda ya kati Aboubakar Ndwata amesema wameweka kituo kimoja cha kupata huduma zote kwa wawekezaji nchini ili mwekezaji anapotaka kuwekeza nchini awakute watoa huduma wote muhimu eneo moja.

Amesema hiyo imepunguza na kuokoa muda kwa wawekezaji wa kutafuta taasisi muhimu zinazohitajika kupitia ili wapate kibali cha kuwekeza nchini.


Post a Comment

0 Comments