BILIONI 25 ZATUMIKA KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA.

 


📌NA DOTTO KWILASA


SERIKALI kupitia Wizara ya afya ,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na Watoto kitengo cha huduma za kinga imesema itaendelea kuboresha huduma za afya nchini  ambapo kwa mwaka 2020 imetoa jumla ya shilingi Bilioni 25 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji na miundombinu ya usafi wa mazingira huku vituo vya afya 893 vikinufaika.

Hatua hii imekuja huku Tanzania ikiwa inaazimisha siku ya mazingira duniani(26/09/2020) yenye lengo la kuikumbusha jamii kulinda na kuboresha afya na mazingira jambo ambalo ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza .

Hayo yamebainishwa jana jijini hapa na Mkurugenzi wa huduma za kinga Dk.Leonard Subi wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa serikali ya awamu ya tano katika eneo la usafi wa mazingira kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020.

Akifafanua,Dk.Subi alisema katika kipindi cha miaka mitano vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vimeboresha huduma za maji na miundombinu ya usafi wa mazingira ni 826 kati ya lengo la vituo 1,000 sawa na asilimia 82.6.

Kwa upande wa shule za msingi Dk.Subi alisema,Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 17.5 kwa ajili ya kuwezesha uboreshaji wa huduma za maji ,vyoo na sehemu za kunawia mikono kwa wanafunzi ambapo kupitia fedha hizo jumla ya shule 602 zimenufaika.

Jumla ya matundu 9712 ya vyoo bora yamejengwa kwa ajili ya wanafunzi 446,155 kwa uwiano wa tundu 1 kwa wanafunzi wavulana 50 na wasichana 40 kwa kila tundu 1,pia sehemu ya haja ndogo kwa wavulana ,vyumba maalumu kwa wasichana kujisitiri na matundu mawili kwa ya walemavu kwa kila shule.
Dk.Subi

Licha ya hayo alisema  Serikali imejenga matundu 526 kwa ajili ya watumishi yaani walimu na wasio walimu huku upatikanaji wa maji safi ukiwa umeboreshwa katika shule hizo 602 na kila shule inapata huduma ya maji wakati wote.

“Fedha hizi pamoja na zile za vituo vya afya zimetolewa na serikali kupitia mradi wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira ”alifafanua Dk.Subi

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi msaidizi ,afya na mazingira Anyitike Mwakitalima alisema mradi wa huduma za maji umetekelezwa katika maeneo ya vijijini na mjini na  kusema kuwa kwa ujumla upatikanaji wa huduma za maji nchini umefikia asilimia 85 Disemba 2019 toka asilimia 70 mwaka 2015 kwa maeneo ya mijini na asilimia 70.1 kutoka asilimia 48 kwa maeneo ya vijijini.

Mwakitalima ambaye pia ni Mkuu wa sehemu ndogo ya maji ,chakula na usafi wa mazingira alieleza kuwa utekelezaji wa afua hizo mbili za maji na usafi wa mazingira umesaidia katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza ambapo hakuna kisa chochote cha mgonjwa wa kipindupindu kuanzia Julai 2019 hadi sasa.

Licha ya hayo alieleza kuwa ,katika kutekeleza mazingira wezeshi ya kiutendaji serikali imepanga kuhakikisha angalau kila mkoa unapata gari moja na kila Afisa afya aliye ngazi ya kata anakuwa na pikipiki .

 

Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments