CHEZA KIDANSI MUSIC AWARDS MSIMU WA PILI KUFANYIKA DODOMA

 


📌NA MWANDISHI WETU

TUZO za muziki wa dansi nchini Tanzania kwa wanamuziki waliofanya vizuri mwaka 2020 zitafanyika jijini Dodoma mwezi Desemba.

Tuzo hizo maarufu kama Cheza Kidansi Music Awards zilizozinduliwa mwaka 2019 zitahusisha vipengele 11.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni ya Cheza Kidansi Entertainment ya jijini Mwanza, imebainika kuwa tuzo hizo zitakuwa na maboresho mengi kwa mwaka huu.

Bernard James amesema vipengele vya mwaka huu ni bendi bora, wimbo bora, video bora, mtunzi bora, mwandaaji bora, mwimbaji bora, rapa bora, hall of fame, chipukizi bora, best collabo na mwanamuziki bora.

Hivi vipengele vimeidhinishwa na academy iliyosheheni wataalamu wa muziki nchini waliokaa pamoja mwaka mzima wakivichambua kwa umakini mkubwa

Bernard James

Amesema baadhi ya vipengele mfano msanii bora, mnenguaji bora, mpigaji bora vyombo, mwanamuziki toka Kongo vimeondolewa ili kuweka chachu kwa vipengele vilivyopitishwa na kukuza muziki wa dansi nchini.

Mkurugenzi huyo wa Cheza Kidansi pia amebainisha kuwa mwaka huu ushindani utakuwa mkubwa sana kutokana na tuzo za mwaka jana kuchochea wanamuziki kutoa kazi nyingi na bora zaidi.

Mfano wa eneo ambalo mwaka huu litakuwa na upinzani mkali ni kwenye rapa bora ambapo marapa wenye majina karibu wote wameshiriki nyimbo nyingi zikiwemo zao na za bendi zingine

Bernard James

Alipoulizwa kwanini tuzo mwaka huu zitatolewa Dodoma, Bernard amefafanua kuwa lengo ni kusogeza tuzo hizi katika mikoa mbalimbali na kuamsha mashabiki wa dansi nchi nzima.

Mwanamuziki mkongwe Nyoshi El Sadaat akipokea
tuzo yake katika msimu wa kwanza wa tuzo za muziki wa dansi.

Kwa upande wa zawadi amesema zawadi ni za aina yake, za kisasa na zitakazowainua zaidi wanamuziki morali na ubunifu.

Kuhusu wadhamini, Mkurugenzi huyo amewaomba wafanyabiashara, wajasiriamali, wadau wa burudani na wamiliki wa makampuni na taasisi mbalimbali jijini Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kudhamini tuzo hizo ili kutangaza pia bidhaa zao, huduma na makampuni kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao itakayotangaza tukio hilo mwanzo hadi mwisho.

Amezitaka bendi na wanamuziki mbalimbali waliotoa kazi mwaka huu kutunza taarifa za kazi zao ili kurahisisha zoezi la kuwapata washindi. Amewaomba pia kutembelea mtandao wa Cheza Kidansi kupata taarifa za tuzo.

Tuzo za Cheza Kidansi tangu zianzishwe mwaka 2019 zimejizolea umaarufu mkubwa huku zikichochea wanamuziki kutoa kazi nyingi na bora mwaka huu.Burudani mbalimbali za dansi zitatolewa sambamba na utoaji wa tuzo hizo mwishoni mwa mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments