MAAFISA MASUHULI KUWASILISHA BAJETI KWA PLANREP



📌NA DOTTO KWILASA

SERIKALI imewaagiza Maafisa Masuhuli wote wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha kuwa, Mpango na bajeti kwa mwaka 2021/22 unaandaliwa na kuwasilishwa kupitia Mfumo  wa Uandaaji Bajeti (PlanRep).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Mary Maganga ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika wakati wa hotuba yake ya uzinduzi na ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya Mfumo mpya wa uandaaji na uwasilishaji wa Bajeti na taarifa za bajeti kielektroniki.

Pia amemwagiza  Msajili wa Hazina kutochambua bajeti yoyote itakayowasilishwa kwake nje ya mfumo huo lengo ni kuhakikisha mfumo huo unatumika kikamilifu.

Mfumo huu wa PlanRep utakuwa kitendea kazi muhimu cha ofisi ya Msajili wa Hazina na naamini hata Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuu zitaweza kutumia mfumo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato.

Mary Maganga

Amesema,hadi kufika mwezi Juni mwaka 2019  Serikali ilikuwa imewekeza katika Taasisi,  Mashirika ya Umma na Kampuni zinazomilikiwa na Serikali kwa hisa chache zipatazo  266   zenye uwekezaji wa kiasi cha shilingi trilioni 59.6 huku akisema mashirika hayo  ni mengi na uwekezaji huo ni mkubwa na unahitaji usimamizi madhubuti utakaowezesha ongezeko la tija katika ukuzaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo ili kuwezesha ufanisi katika usimamizi wa Mali za Umma ilihitajika kuwa na mifumo madhubuti ya kielektroniki itakayorahisisha usimamizi wa rasilimali hizo lakini uwepo wa mifumo hiyo utapunguza upotevu wa mapato,kuimarisha na kuchochea uwajibikaji, kuimarisha uchambuzi wa bajeti na ufuatiliaji na hatimaye kuongeza mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

 “Hivyo basi, mfumo huu wa PlanRep utakuwa kitendea kazi muhimu cha ofisi ya Msajili wa Hazina na naamini hata Wizara na Taasisi nyingine za Serikali kuu zitaweza kutumia mfumo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato,alisema na kuongeza kuwa;

“Wizara ya Fedha na Mipango ilipopata taarifa kuwa umejengwa  mfumo wa bajeti utakaotumika katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, tulipata faraja kwa kuwa mfumo huo wa Bajeti utakuja kuunganishwa na mfumo wa ulipaji Serikalini na  hivyo kuwezesha kudhibiti matumizi ya fedha za umma nje ya mipango na bajeti iliyoidhinishwa,na ninachowasisitizia ni kuhakikisha kuwa mifumo hii inatumika ipasavyo.”anasema

Awali akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo Msajili wa Hazina Selemani Mbutuka amesema jumla ya washiriki 944 kutoka katika Taasisi na Mashirika ya Umma 236 watajengewa uwezo wa kutumia mfumo huo.

Amesema,mfumo huo utatumika katika Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma huku akisema , tayari ulishaanza kutumika na Mamlaka za Serikali za Mitaa tangu mwaka 2017/18, mfumo ambao uliboreshwa ili uweze kutumika na kila Taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Msajili wa
Hazina.

Ameongeza kuwa uwepo wa mfumo huo utasaidia kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za Umma katika Mashirika na Taasisi za Umma pamoja na upatikanaji wa taarifa za uhakika na kwa wakati; kupunguza gharama kubwa za fedha za umma katika ununuzi, uundaji, usimikaji, uendeshaji
na usimamizi wa mifumo hiyo, pamoja kupunguza utitiri wa mifumo ya kibajeti ya kieletroniki iliyoanzishwa bila kupata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni msimamizi mkuu wa fedha na mali za umma.

Lakini pia  uwepo wa mfumo huu utasaidia sana kuongeza ufanisi na tija katika usimamizi na ufuatiliaji wa uwekezaji wa Serikali katika Taasisi, kuboresha utendaji kazi wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza makusanyo ya serikali kutoka katika vyanzo vyake visivyo vya kodi.
Selemani Mbutuka

Hata hivyo amesema,pamoja na kzinduliwa kwa mfumo huo lakini pia Ofisi ya  Msajili wa Hazina pia imeendelea na juhudi za kuimarisha utendaji kwa njia ya kielektroniki ambapo imetengeneza na inaendelea na utengenezaji wa Mifumo  mbalimbali ikiwemo Mfumo wa ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa za fedha , Mfumo wa Bodi za Wakururugenzi  na Mfumo wa Ufuatiliaji mali za Serikali .

 


Post a Comment

0 Comments