MJUE BIBI TITI MOHAMED:SHUJAA WA KIKE ALIYEPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA.

 


📌NA DOTTO KWILASA.

KILA ifikapo Disemba tisa ,Tanzania huadhimisha uhuru wa Tanzania Bara ambapo zamani ilikuwa ikijulikana kama Tanganyika kabla ya kuungana na visiwa vya Zanzibar na kuunda neno huru Tanzania.

Ikiwa imebaki miezi miwili kuingia katika kipindi cha  historia ya uhuru wa Tanzania Bara uliopatikana tangu mwaka 1961 na kuifanya Tanzania kuwa huru kwa miaka 56 sasa,ni wazi kuwa jamii inapaswa kuwakumbuka na kuwaenzi wanawake waliopigana kufa na kupona kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za kuikomboa Tanganyika.

Wapo wanawake wengi waliojitoa kuipigania nchi hii ya kizalendo ambao majina yao yamo katika historia.

Hata hivyo michango mingi  ya wazalendo wanawake imefichwa na kuwafanya  wasijulikane kabisa katika historia japo tunapaswa kuwashukuru na kuzidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu.

Hivyo basi,hatuwezi kuuzungumzia uhuru wa Tanzania bila kuwahusisha wanawake waliochochea maendeleo ya kuwa na Taifa huru.

Hapa namaanisha hatuwezi kuiadhimisha siku hii bila kumkumbuka mwanaharakati  mmoja wa wanawake wa kwanza wazalendo  kujiunga na harakati za kuikomboa Tanganyika  na huyu si mwingine ni Bibi Titi Mohamed .

Bibi Titi Mohammed ni jina linalojulikana kwa wakongwe huku vijana wa kizazi cha sasa wengi wao hawamjui wala kufahamu harakati zake katika ukombozi wa Tanganyika.

Titi Mohamed Salim Mandwanga alizaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1926 ,na tarehe 5 Novemba mwaka 2000 alihitimisha safari yake ya kuishi duniani kama ilivyoandikwa katika vitabu vyote vya dini.

Katika maisha yake Mama huyu alipenda uhuru na haki na kuamua kuvisimamia vitu hivi kwa vitendo  na kuamua kujiingiza kwenye masuala ya siasa.



Siasa ilimweka akawa  rafiki wa karibu wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere aliyetambulishwa kwake mwaka wa 1954, na dereva wa  familia ya Rais huyo kutokana na imani ya usawa aliyokuwa nayo Baba wa Taifa.

Kwa wakati ule  wanawake kujulikana ilikuwa ni mtazamo mbaya kwa jamii kwani jamii ilijiwekea imani kuwa kazi kubwa ya mwanamke ni kushughulikia familia pekee.

Titi Mohamed alikuwa mmoja wa wanachama waanzilishi wa TANU(Tanganyika African National Union), ambacho kilikuwa chama kikuu cha kisiasa ndani ya Tanzania , na alifanya jukumu kubwa katika kupambana na uhuru wa Tanzania.
Kutokana na kipaumbele kikubwa cha sera ya Nyerere, aliwahimiza wanawake ikiwa ni pamoja na kuihimiza jamii kutambua kuwa binadamu wote ni sawa hivyo kumtoa Bibi Titi kwenye jukwaa alilohitaji ambapo  alikuwa kiongozi wa mlengo wa wanawake wa TANU, yaani Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).

 UWT ilikuwa chanzo kikubwa cha uwezeshaji kwa wanawake nchini Tanzania ambapo kilileta  mafanikio ya ajabu na kutoa historia iliyokuwa imezoeleka ya  kuwadhoofisha wanawake na kuwaona hawafai.

 Hata hivyo ,mnamo Oktoba 1969, Bibi Titi, na Waziri wa zamani wa Kazi Michael Kamaliza walikamatwa, pamoja na maafisa wa jeshi wanne, wakishtakiwa kwa kupanga mpango wa kupindua serikali kutokana na kutokubaliana kwa baadhi ya mambo ndani ya chama hali iliyomfanya kuhukumiwa kifungo cha maisha.

Taarifa zinaeleza zaidi kuwa ,miaka miwili baadaye yaani  mwezi wa Aprili 1972, Bibi Titi alipokea msamaha wa Rais.

 Baada ya kutolewa kwake, machungu  na mateso yalianza kwa mwanamke huyu mzalendo (Bibi Titi) ambapo alianza kuishi  maisha ya kutengwa na jamii yake iliyokuwa ikimpenda mwanzo.

 Unajua nini kilitokea? washirika wake wa kisiasa walimpinga, rafiki zake wengi walimkataa na kumwona kuwa hafai kuambatana nao lakini kubwa zaidi ni hili la mume wake aliyempenda na kumuamini sana  kumtaliki kutokana na mfumo dume uliokuwapo wakati ule hali iliyozidi kuamsha ari ya mwanamke huyu katika kupambana kwa nguvu zote kusimamia kile alichokiamini kuwa kitamfanya kuwa huru.



Hayo ni baadhi tu ya mambo yaliyomtokea mwanaharakati huyu mwanamke anayetazamwa na wegi kama mzalendo wa kweli na hatimaye kufanikiwa kufikia malengo ambapo mnamo mwaka 1991, wakati Tanzania ilipokuwa ikisherehekea miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi kinara wa ushindi na kuwahamasisha wanawake wengine kuiga mfano wake.

Hata hivyo kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho,mnamo Novemba 5, 2000 mama huyu alifariki kwenye hospitali ya huduma ya afya  huko Johannesburg  nchini Afrika ya Kusini ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Kutokana na umuhimu wake katika Taifa hili ambalo kwa sasa ni huru ,Serikali iliona ni vema kumuenzi kwa namna ya pekee ili kumhifadhi katika kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

 Moja ya barabara kuu za jiji la Dar es Salaam inaitwa jina la Bibi Titi Mohamed  kwa heshima ya mafanikio makubwa yaliyotolewa na yeye kuelekea uhuru wa Tanganyika.

 Kubwa zaidi ni matumizi ya lugha ya kiswahili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo inasemekana akiwa waziri alishauri lugha hii kutumika na kuwaweka watu pamoja badala ya kiingereza .

Huyo ndiye shujaa wa kike aliyepigania uhuru wa Tanganyika,nakukumbusha msomaji wa makala haya ya Sauti ya Mwanamke kuwa vielelezi vingi katika makala haya ni kwa hisani ya mtandao.

 Kwa maboresho ya ukurasa huu usisahau kuwasiliana nasi kupitia barua pepe habaricentral4@gmail.com au kupitia dottokwilasa@gmail.com.

 


Post a Comment

0 Comments