MPANGO MKUU WA SEKTA YA FEDHA WA MIAKA 10 WAZINDULIWA DODOMA



📌NA PENDO MANGALA
WIZARA ya Fedha na Mipango imezindua mpango wa Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2019/2020 hadi 2029/2030 ambao  umelenga  kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wote zikiwemo za bima.

Akizindua mpango huo leo Sept.17,2020 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dotto James,Naibu Katibu Mkuu Mary Maganga amesema  mpango huo utaongeza wigo katika upatikanaji wa  huduma za mikopo ,akiba ,uwekezaji na kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na sekta ya viwanda.
Amesema,mpango huo umeandaliwa ili utumike kama nyenzo ya kutatua changamoto zilizopo ambapo pamoja na mambo mengine  pia  umelenga kuongeza upatikanaji mitaji ya muda mrefu, upatikanaji huduma jumuishi za fedha na kulinda watumiaji wa huduma za fedha .

Pia amebainisha kuwa mpango huo wa miaka 10 unalenga  kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha ,kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha ,kudhibiti  utakatishaji fedha haramu   na kuweka mazingira wezeshi ya sheria ,kanuni ,taratibu na miongozo katika sekta ya fedha.
Kwa upande wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti amewataka kuona fursa zilizopo katika mpango huo na kujipanga katika kuboreshan maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiutafiti ili kuhakikisa sekta hiyo inaendelea kuwa yenye ushindani na kuweza kuhimili mabadiliko ya nyakati kwa wepesi na weledi.

Akitoa maelezo ya mpango huo, Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha  Dkt.Charles Mwamwaja amesema wakati wa maandalizi,timu ya wataalam wa Mpango huo ilifanya mapitio kwenye nyaraka mbalimbali zikiwemo taarifa za maboresho ya sekta ya fedha ,Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025,Dira ya Taifa ya Maendeleo Zanzibar ya  mwaka 2020 na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza umasikini Zanzibar (ZSGRP III) .

Pia  Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2016/17-2020/21 na taarifa ya Programu ya Tathimini ya Sekta ya Fedha yam waka 2018 kwa lengo la kupata matokeo zaidi katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa.

Post a Comment

0 Comments