UHABA WA MAJI WATESA WAKAZI WA MTUMBA




📌NA DOTTO KWILASA

BAADHI ya Wakazi Kata ya Mtumba jijini Dodoma wameuomba uongozi wa serikali ya mtaa huo kuwatatulia changomoto ya uhaba wa maji ambayo imedumu kwa muda mrefu .

Aidha wakazi hao waliopo karibu na mjini wa serikali wamesema kuwa  hali hiyo inawasababisha kushindwa kufanya  shughuli zao kimaendeleo na kutumia mda mwingi kutafuta maji.

Wakiongea  jana jijini hapa wananchi hao wamesema  kumekuwa na changomoto kubwa ya maji kwa kipindi cha miezi miwili sasa.

Hagulwa Manase amesema uhaba wa maji unawakosesha wanawake wengi kushindwa kutimiza majukumu yao kifamilia.

Muda mwingi maji yanatoka kwa nusu saa kisha yanakata,watoto wetu wanashindwa kupata huduma za malezi ,tunaomba Serikali utusaidie

Naye Pendo Manga Abraham ametumia nafasi hiyo kuomba uongozi wa mtaa huo kuhakikisha wanatoa ratiba ya maji ili kila mwananchi aweze kupata maji .

Kuna muda maji yanatoka wakati ambao watu hawapo majumbani kwa kuwa tumezoea maji hayatoki Sasa ukitoka unakuta maji yamekata

Pamoja na hayo amesema hapo awali maji yalikuwa yakitoka bila kukatika na kufanya jamii ya eneo hilo kufanya shughuli zao za uzalishaji mali bila vikwazo .

"Tunasikitika kuona hali imebadilika ghafla baada ya maji kukatika kila wakati na kujikuta tukikosa maji,Kuna wakati maji hayatoki kabisa kwa muda wa wiki hapo tunaanza kununua maji ya kisima kwa Shilingi 300,"amesema.

Licha ya hayo wakazi hao wa Mtumba wameongeza kuwa licha ya eneo hilo kuwa maarufu kutokana na  kuwepo kwa ofisi nyingi za serikali (Mji wa serikali) lakini eneo muhimu kama hilo linakuwa na changamoto ya maji.

Kutokana na hayo Mwenyekiti wa mtaa huo Robert Chigugude amekiri kuwepo kwa changomoto hiyo huku akisema   imetokana na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma hiyo jambo ambalo limesababisha pampu inayosukuma maji kushindwa kuhimili idadi ya watumiaji wa sasa.

Aidha amewataka wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikishughulikia changamoto hiyo kwani wamepeleka taarifa kwa mamlaka ya usimamizi wa maji vijijini (RUWASA) na kwamba matengenezo yanatarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia  sasa.

Niwatoe wasiwasi wananchi wangu,naomba wawe wavumilivu kwani tuna mpango wa kusahihisha changamoto zote zinazotokana na maji

Robert Chigugude

 


Post a Comment

0 Comments