WAMILIKI LESENI MADINI WAPEWA MIEZI MIWILI YA UHAKIKI



📌NA JASMINE SHAMWEPU
WAMILIKI wa leseni za madini wametakiwa kufika katika ofisi za kanda zao kwa ajili ya kuhakiki leseni bila kufanya hivyo watanyang’anywa leseni hizo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma,Katibu Mtendaji Tume ya Madini Profesa Shukrani Manya amesema zoezi la uhakiki wa leseni za madini nchini limeanza rasmi wiki hii  na linatarajiwa kuhitimishwa Novemba 2 mwaka huu.
Amesema,Tume hiyo imapanga kuendesha zoezi la uhakiki wa leseni zote za madini kwa kipindi hicho kirefu ili kutoa mwanya kwa kila mmiliki wa leseni kupata muda wa kuhakiki leseni yake huku akisema wamiliki wote wanatakiwa kufika kwenye ofisi za madini za hizo za madini wakiwa na leseni zao halali na taarifa muhimu zinazohusiana na leseni zao.
Amesema mambo muhimu ya kuhakiki ni pamoja na uhalali wa leseni husika,ili kujua leseni ambazo hazijaendelezwa na leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka  .
Aidha amewataka wamiliki  wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye mapungufu kuyarekebisha ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Prof.Manya amesema miongoni mwa  mapungufu hayo ni pamoja na maombi yaliyokosa viambatanisho muhimu,maombi ambayo hayajalipiwa ada na waombaji ambao walikidhi vigezo vya kupewa leseni lakini kwa namna moja ama nyingine hawajalipa ada za maandalizi pamoja na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa na lakini hajachukua.
Leseni za walioomba uchimbaji wa kati zipo 15 na leseni za utafutaji madini zipo 96, mmiliki au mwombaji atakayeshindwa kuwasilisha mapungufu yaliyoainishwa baada ya uhakiki zitafutwa kwa mujibu wa sheria.
Profesa Manya
Kwa mujibu wa Profesa huyo maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji yenye mapungufu yataondolewa kwenye mfumo wa uombaji leseni ili wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.
Pia ametumia fursa hiyo kuwaagiza maafisa madini wakazi wote waweke dawati la uhakiki katika ofisi zao kwa kipindi chote cha zoezi la uhakiki huo.
Awali Kamishina wa  Tume ya Madini Profesa Abdulkareem Mruma ameoneshwa kushangazwa na kitendo cha wamiliki wa leseni mbalimbali kupewa leseni hizo baada ya kukidhi vigezo lakini hawajachukua leseni zao.
Profesa Mruma pia amesema Wizara ya Madini tayari imeshatunga na kukamilisha kanuni za uongezaji thamani madini za mwaka 2020 kanuni ambazo amesema ndio  zitatumika katika kusafirisha madini ambayo  yameongezwa thamani.
Amewataka wateja watumie kanuni hizo ili waweze kupeleka nje ya nchi madini ambayo yameongezwa thamani huku akiwaomba ambao hawakusafirisha madini siku nyuma watumie kanuni hizo katika kuongeza thamani na ubora kwa viwango vilivyoainishwa.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2017 Serikali ilifanya marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo pamoja na mambo mengine ilizuia usafirishaji makinikia na madini ghafi kwenda nje ya nchi baada ya kubaini udanganyifu na upotevu mkubwa wa mapato ya serikali wakati wa usafiorishaji wake.

Post a Comment

0 Comments