📌NA DOTTO KWILASA
WAZAZI wenye watoto
wanaoishi na ugonjwa wa Sikoseli wameiomba Serikali kuona haja ya
kuongeza madaktari maalumu wenye ujuzi wa ugonjwa huo ili kupunguza madhara kwa
wagonjwa.
Hayo yameelezwa jana
jijini Dodoma wakati wa kufunga mwezi wa uhamasishaji jamii kuhusu ugonjwa
wa sikoseli.
Mmoja wa mama hao
Zuhura Makuka amesema vituo vingi vya kutolea huduma za afya nchini hazina
wataalamu wa kutosha wa ugonjwa sikoseli na hivyokusababisha wagonjwa
wengi kukosa huduma kwa wakati.
Hospitali nyingi hazina kliniki maalumu za kutolea huduma za sikoseli hivyo ukienda unakutana na wahudumu wa afya ambao hawana uelewa,hali hii inatuvunja moyo
Licha ya hayo ameeleza
kuwa baadhi ya watoa huduma za afya nchini wakiwemo madaktari hawana
uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa wa sikoseli hali inayosababisha unyanyapa
kuendelea kuwepo katika jamii .
Amefafanua kuwa wao
kama wazazi wenye Watoto wa ugonjwa huo wamekuwa na wakati mgumu wanapokutana
na vikwazo hivyo ambapo hufika wakati wanakata tamaa ya kuendelea
kuwahudumia Watoto wao.
Kutokana na hayo
,Wizara ya afya ,Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza,kutoka
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto,Dk.James Kiologwe
alisema ,Serikali kupitia wizara hiyo tayari imeafanya mkakati wa kutatua kero
zote zinazohusu ugonjwa huo.
Tayari tumechukua hatua kadhaa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kuunda kikosi kazi cha wataalamu wa kukabiliana na ugonjwa huo,tunaamini Htua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa uhaba wa wataalamu wa sikoseli.
Hata hivyo amesema pia
mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila Hospitali ya Mkoa inakuwa na Kliniki kwa
ajili ya kupima ugonjwa wa Sikoseli.
Hata hivyo ameiasa
jamii kuzingatia uchunguzi wa afya kabla ya kuingia kwenye mahusiano ili
kuepuka kupata watoto wenye ugonjwa wa sikoseli.
Akizungumza kwa niaba
ya Mganga Mkuu wa Serikali,Profesa Abeid Makubi ,Dk.Kiologwe
amesema,utafiti unaonesha kwamba kila watoto 100 waliopimwa
ugonjwa wa Sikoseli 15 ama 20 wamekutwa na vinasaba vya ugonjwa huo huku Kanda
ya Ziwa ikitajwa kuwa na wagonjwa wengi.
Aidha amesema katika
utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015 unaonesha
kwamba kati ya watoto 100 waliopimwa ugonjwa wa Sikoseli watoto
kati 15 mpaka 20 wamekutwa na vinasaba vya ugonjwa wa Sikoseli.
Dk.Kiologwe pia
alisema jumla ya watu 1000 huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila siku
duniani.
Mkurugenzi huyo
alieleza kuwa Tanzania ni nchi ya tano duniani kuwa na idadi ya wagonjwa wengi
wa Sikoseli huku ikishika nafasi ya nne barani Afrika.
Nchi zenye wangonjwa wengi duniani ni Nigeria,India,Kongo,Angola na Tanzania,ambapo kwa Afrika Tanzania inashika nafasi ya nne hali inayopaswa kutiliwa mkazo zaidi kuhakikisha ugonjwa huu unazuiwa
Amesema ,Tanzania
,kila watoto 100 wanaozaliwa nchini ,8 Kati yao wana ugonjwa wa Sikoseli.
Pamoja na hayo
ameongeza kuwa,Licha ya juhudi nyingi zinazofanywa na wizara ya Afya Katika
kuelekeza nguvu za uelimishaji jamii juu ya ugonjwa huo ,jamii bado haina
uelewa wa kutosha hali inayosababisha unyanyapaa kwa waathirika wa ugonjwa huo.
Kwa upande wake,Rais
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ambaye pia ni Daktari bingwa wa
Magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dk.Elisha Osati
amesema walitumia mwezi mmoja kutoa elimu kwa jamii katika Mikoa ya Kanda
ya Ziwa ambapo kati ya watoto 1,800 waliowapima 360 wamewakuta na
vinasaba vya ugonjwa huo.
Tumejitahidi kufanya mambo mengi kwanza kutoa elimu, tumepita katika shule 15 zilizopo Kanda ya Ziwa,tumewafikia wanafunzi 10,000 tumewapa elimu.
Hata hivyo amesema
katika Hospitali 6 walizozitembelea Kanda ya Ziwa ni mbili pekee ndizo
zenye Kiliniki ya kupima ugonjwa wa Sikoseli huku akikiri wagonjwa wengi kuwa
katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande
wake,Daktari bingwa wa Magonjwa ya Watoto,kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma,Dk.Halima Kassim amesema wameanzisha Kiliniki wa ugonjwa huo mkoani
Dodoma baada ya kugundua kuna watoto wengi wenye ugonjwa huo.
0 Comments