WENYE ULEMAVU WAOMBA KUPATIWA ELIMU YA MAGONJWA YA MLIPUKO.

 


📌NA DOTTO KWILASA

 KUTOKANA na ongezeko la watu kunakotokana na kukua kwa Jiji la Dodoma ,baadhi ya watu wenye ulemavu wameiomba Serikali kuwapa uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Walemavu hao wamesema bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo pamoja na kutokuwa na uelewa wa jinsi yanavyoambukiza.

Licha ya serikali kuchua tahadhari kupitia Wizara ya afya ,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na Watoto kitengo cha huduma za kinga kutoa elimu juu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kwa jamii ,watu wenye ulemavu wamesema bado wapo nyuma kwa kukosa  uelewa wa kutosha kuhusu namna bora ya kuwaepusha na magonjwa.

Kutokana na hayo,baadhi ya wenye ulemavu wameishauri Serikali kuona haja ya kuboresha namna ya uelimishaji unaotumika Katika jamii ili elimu hiyo iwafikie watu wote katika makundi maalumu.

Saimon Kalinga  mkazi wa mtaa wa Chan'gombe Jijini hapa amesema kuwa,elimu ya masuala ya magonjwa ya mlipuko imekuwa ikitolewa kwa ubaguzi jambo linalowatia hofu .

Wengi wetu tunayaskia tu hayo magonjwa ya mlipuko lakini ukituuliza magonjwa hayo yanaletwa na nini hatujui kabisa.

Saimon Kalinga 

Naye Zamda Issa mkazi wa mtaa wa  Makulu anasema kuwa watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa kipaumbele cha elimu ya magonjwa ya mlipuko ili kupunguza madhara ya ugonjwa huo yanapojitokeza.

"Waelimishaji wa masuala ya afya wengi wao linapokuja suala la uelimishaji kwa jamii huwa wanasahau kabisa kuwa Kuna kundi la walemavu,wanapaswa kuelewa kuwa kuwaelimisha baadhi tu ya watu haitasaidia Ikiwa wengine hawana elimu,"anafafanua.

Pamoja na hayo amesema Kufikiwa kwa walemavu kutasaidia kuiepusha jamii yote na magonjwa Kama ya kuhara na kipindupindu na kufafanua   kuwa Kuna baadhi ya familia wanapata magonjwa ya mlipuko Kutokana na kuwatenga Wenye ulemavu.

"Mimi pia ni sehemu ya jamii,naishi katika familia ,Sasa unapoelimisha wengine na kuniacha mimi kwa kuwa Sina uwezo wa kutembea unaiumiza jamii yote kwa kuwa nitakaa mjinga lakini pia ujinga wangu utawaumiza wengi ,"anasema.

Kutokana na hali hiyo,Wizara ya afya imesema imechukua hatua kwa kuongeza juhudi katika kulinda na kuboresha afya ya watu wenye ulemavu kwa kujielekeza katika eneo la afya ya mazingira ambalo ni muhimu kwenye kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza.

Katika kulisimamia hilo,wizara hiyo kwa kusimamia utekelezaji wa kampeni ya Taifa ya usafi wa mazingira,imejikita kuhamasisha jamii kwa ujumla kujenga na kutumia vyoo bora sambamba na maeneo yanayotoa huduma za kijamii kwa kuzingatia miundombinu wezeshi kwa walemavu.

Mkurugenzi wa huduma za Kinga Dk.Leonard Subi amesema katika kuhakikisha wenye ulemavu wanakuwa salama na kuepukana na magonjwa ya mlipuko,Serikali ina mpango endelevu wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko katika mkoa wa Dodoma kulingana na ukuaji wake.

Licha ya hayo Dk.Subi ametaja mpango huo endelevu kuwa ni pamoja na kuwezesha uboreshaji huduma za maji na vyoo ambapo jumla ya shule 602 zimenufaika kwa kujengewa matundu mawili ya walemavu kwa kila shule.

Tutaendelea kuboresha huduma za afya na mazingira nchini  ambapo kwa mwaka  2020 serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 25 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji na miundombinu ya usafi wa mazingira na kunufaisha vituo vya afya 893

Dk.Subi.

Hata hivyo anaitaka jamii kuendelea kujilinda na kuboresha afya na mazingira jambo ambalo ni muhimu katika kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kwa kufanya usafi kila Mara na kutumia maji Safi na kwa usalama wa afya zao .

"Tunawatumia wanafunzi kama mabalozi wa usafi wa mazingira ,kwa kuzingatia maisha ya usafi wa mazingira shuleni utasaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko,amesema na kuongeza;

“Katika kujikita kuboresha mazingira jumla ya matundu 9712 ya vyoo bora yamejengwa kwa ajili ya wanafunzi 446,155 kwa uwiano wa tundu 1 kwa wanafunzi wavulana 50 na wasichana 40 kwa kila tundu 1,pia sehemu ya haja ndogo kwa wavulana ,vyumba maalumu kwa wasichana kujisitiri na matundu mawili kwa ya walemavu kwa kila shule”amesema.

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi msaidizi ,afya na mazingira Anyitike Mwakitalima amesema Serikali kupitia wizara hiyo imeandaa  mradi wa huduma za maji unaotekelezwa katika maeneo ya vijijini na mjini na  kusema kuwa hali hiyo itasaidia kuboresha mazingira na kuepusha magonjwa yasiyo ya lazima kwa jamii.

Mwakitalima ambaye pia ni Mkuu wa sehemu ndogo ya maji ,chakula na usafi wa mazingira ameeleza kuwa utekelezaji wa afua hizo mbili za maji na usafi wa mazingira utawasaidia walemavu na jamii kwa ujumla katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza na mlipuko.

"Maji ni uhai ,tunapoweka mazingira safi ,maji yanakuwa salama zaidi ,niiombe jamii kutumia maji Safi na sabuni kunawa mikono kuua vijidudu vya maradhi,"anasistiza .

 

Post a Comment

0 Comments