MAGONJWA YA MLIPUKO YANASABABISHWA NA TABIA YA BINADAMU.

 


📌FAUSTINE GIMU GALAFONI

WANANCHI katika maeneo mbalimbali jijini Dodoma wamesema kuwa magonjwa ya Mlipuko mara nyingi husababishwa na tabia za binadamu zikiwemo utiririshaji wa maji machafu kutoka chooni na kuyaacha yakitapakaa barabarani.

Wakizungumza na CPC Blog jijini Dodoma baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa mara nyingi tabia mbalimbali za wananchi zimekuwa ni chanzo ya magonjwa ya mlipuko ikiwepo kipindupindu na kuhara.

Akizungumza na CPC Blog mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Bonanza jijini hapa Cosmas Mathias amebainisha kuwa   pamekuwepo na tabia ya baadhi ya wananchi kuzibua vyoo vyao hali ambayo husababisha maji machafu kuzagaa na kutiririka barabarani jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wapita njia wakiwemo watoto na watu wazima.

“Kwa kweli hali kama hii si nzuri maana unavyoona maji haya yamekosa mwelekeo na kusababisha kuzagaa ovyo njiani kuna sehemu choo kimezibuliwa, sisi wananchi wakati mwingine tumekuwa tukisababisha sisi wenyewe mlipuko wa magonjwa na kuilaumu serikali bure na ukiangalia sasa tunaelekea kwenye mvua za masika na hali itakuwa mbaya zaidi.” Amebainisha Mathias

Mtandao huu umepata fursa ya kuzungumza na mmiliki wa nyumba ambayo imekuwa kero kwa utiririshaji wa maji machafu mtaani hapo jina lake limehifadhiwa alibainisha kuwa eneo nyumba ilipo kuna unyevunyevu ndio maana hutokea hali kama hiyo ya choo kujaaa na inapotokea hali kama hiyo wakati mwingine huwa hana fedha kukodi gari la kufyonza uchafu chooni

“Kwa kweli katika eneo hili kuna changamoto pia ya chemchem[unyevunyevu]sasa inapotokea hali kama hii wakati mwingine pesa sina lakini huwa najitahidi na kama unavyoona kuna unafuu, na kitu kingine njia zinatakiwa ziboreshwe pawe na mifereji ya kupitisha maji taka maana mji huu   unazidi kukua    na hakuna mtu anayependa mwenzake apate ugonjwa”amebainisha.

Kwa upande wake mjumbe wa serikali ya mtaa huo kitengo cha Afya Bi.Kalunde Issa Tumbo amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika mtaa huo ambapo amebainisha kuwa  jambo la utiririshaji maji taka katika mtaa huo imekuwa changamoto .

“Kwa kweli katika mtaa huu pamekuwa na changamoto hata wakati nakuja ofisini nimekuta kuna maji taka yaliyochangamana na vinyesi yanazagaa barabarani na mara nyingi tumekuwa tukisuluhisha migogoro hii kwani wananchi wamekuwa wakileta kero “amesema.

Hata hivyo,Bi.Tumbo amesema usafi ni wajibu wa kila mtu na usafi ni amri na wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kwa wamiliki wa nyumba ambapo wamekuwa wakikaa muda mrefu bila kuzibua vyoo vyao.

Pia, amebainisha kuwa maji taka yaliyoambatana na vinyesi kutapakaa ovyo barabarani kuna sababishwa na sababu kuu mbili zikiwemo uzembe wa wamiliki wa nyumba kukaa muda mrefu bila kuzibua vyoo pamoja na miundombinu ya mfumo wa maji taka kuchakaa.

 

 

Katika hatua nyingine Mganga Mkuu wa Serikali,Prof. Abel Makubi amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwakuzingatia suala la usafi kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo mbalimbali hapa nchini.

Prof.Makubi amebainisha hayo hivi karibuni  Jijini Dodoma wakati  akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanachi kuchukua tahadhari na njia za kuepuka magonjwa ya mlipuko katika kipindi cha mvua za Vuli kuelekea Masika  ambazo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Prof.Makubi amesema kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa magonjwa kama ya kuhara ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu, kuhara damu na yale yanayoenezwa na Mbu ikiwemo ugonjwa wa Malaria na Dengue endapo wanachi hawatazingatia kanuni za afya na kuchukua tahadhari mapema.

“Wote tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa mioundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha na kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii inaweza kuhatarisha afya ya jamii na kuongeza uwezekano wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko,”amesema.

Aidha amesema kwa sababu hiyo Wizara imeona bora kutoa taarifa na tahadhari kwa umma ili kuweza kuchukua tahadhari na kuelekeza njia za kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.

 “Ili kuweza kuandika historia ya kutokomeza kabisa kipindupindu na magonjwa mengine hatuna budi kukumbushana na kuchukua tahadhari kwa kila mwanachi, Taasisi na viongozi wa ngazi zote ili kujikinga na kuzingatia kanuni za afya kwa kuchemsha maji ya kunywa au kutibu kwa dawa maalum kama waterguard kabla ya kuyatumia na kuhakikisha maji ya kunywa na yale ya matumizi ya nyumbani yanahifadhiwa katika vyombo safi,” amesisitiza.

 Prof.Makubi ameendelea kufafanua ni vyema kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira  yasiyo safi na salama, kutumia vyoo ipasavyo na kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni mara kwa mara  kabla ya kula baada ya kutoka chooni,baada ya kumuhudumia mgonjwa pamoja na kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula.

Pia amewataka wananchi kuongeza usimamizi wa usafi wa ujumla na mikono katika maeneo ya mikusanyiko kama mashuleni, Vyuo na Masoko, kutotapisha vyoo au kutiririsha maji taka, kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu muda wote na kutumia ipasavyo vyandarua

Aidha, amewataka waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa,wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo lililo chini yao haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko.

Hata hivyo. Prof.Makubi amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto hakujaripotiwa  mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa  kipindi cha mwaka mmoja na nusu hadi sasa.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti magonjwa haya ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao ulikoma Julai 2019 na hii inatokana na jitihada kubwa za maboresho ya miundombinu ikiwemo kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na ushirikiano mzuri wa wanachi,” amesema.

 

Wakati huohuo, katika kuadhimisha  miaka 21 ya Kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarange Nyerere  Octoba 14, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na kampuni ya Green Waste walifanya shughuli mbalimbali za usafi wa Mazingira katika kata ya madukani jijini hapa.

Akizungumza na Mtandao huu mara baada ya kufanyika kwa usafi huo Afisa Mazingira wa Jiji la Dodoma Bwana Ally Mfinanga amesema walisafisha mitaro ya maji ya mvua kwani wakati mwingine huwa kuna changamoto ya taka ngumu hivyo kusababisha kuziba ndio maana wamefanya usafi huo kwaajili ya kuzibua mifereji ili maji yaweza kupita kiurahisi bila kuleta athari hususani kwa wafanyabiashara na wakazi ambao wako kata hiyo.

Alisema mifereji hiyo imejengwa mahususi kwaajili ya kupitisha maji ya mvua na si kwaajili ya kutupa takataka.

Kwa upande wake Sebastian Mkomagi ambaye ni Mwakilishi wa Kampuni ya Green waste inayojishughulisha na ufanyaji usafi katika jiji la Dodoma alisema wao wakiwa kama wadau wa mazingira wameamua kuadhimisha siku hiyo kwaajili ya kufanya usafika lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira katika hali ya usafi.

 

 Katika hatua nyingine ,mratibu wa shughuli za vijana kutoka Raleigh Tanzania Society Jonathan Ngonyani  alisema ni vyema jamii pia ikawa na tabia ya kusoma sheria mbalimbali ikiwemo hizo za mazingira kuendelea kuyatunza mazingira kikamilifu na kushiriki kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na vifungu vya sheria.

Post a Comment

0 Comments