THBU YAWATAKA WADAU WA UCHAGUZI KUZINGATIA MAADILI, KUHESHIMU HAKI ZA BINADAMU

 


📌NA DOTTO KWILASA.

 TUME ya haki za binadamu na utawala bora (THBU) imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulipa uzito tukio la uchaguzi mkuu kwa kukubali kutoa fedha za kugharamia ili wananchi waweze kutimiziwa haki yao ya kikatiba.

Hayo yamezungumzwa jijini hapa na Mwenyekiti wa Tume hiyo (THBU)Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa tamko la tume hiyo kuelekea  siku ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu.

Akitoa tamko hilo,Mwenyekiti huyo amesema ,Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar imefanya maandalizi mazuri  kwa mwendelezo wa utoaji elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu uchaguzi mkuu na kwa kusimamia vyema hatua zote za  mchakato wa uchaguzi kwa weledi huku zikizingatia sheria na kanuni za nchi, haki, usawa, usalama na amani. 

Kutokana na hayo Jaji huyo mstaafu ametoa wito kwa wadau mbalimbali Wanapotekeleza majukumu ya Uchaguzi mkuu wazingatie maadili, waheshimu haki za binadamu  na misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi makubwa ya nguvu yasiyokuwa ya lazima.

Tume inawaasa wananchi wote raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutimiza wajibu wao wa kuzingatia sheria na kanuni za nchi kwa kuhifadhi amani katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi kwa maslahi ya Taifa.
Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu

Akiongea kwa niaba ya THBU,Mwaimu anasema Watanzania wote waliotimiza vigezo kwa mujibu wa sheria, wanapaswa kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kuwachagua Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

“Hatua hii muhimu imefikiwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa miezi kadhaa uliohusisha hatua za uhuishaji wa madaftari ya kudumu ya wapiga kura, uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali na kampeni”amesema.

Licha ya hayo,Mwaimu amesema tume hiyo inalipongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda usalama wa raia na mali zao katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

Vilevile, Tume inavipongeza vyombo vya habari kwa kuzingatia haki ya kikatiba ya wananchi kwa kuwahabarisha kuhusu matukio na sera zilizokuwa zinanadiwa na wagombea na vyama vyao na elimu iliyokuwa ikitolewa na wadau mbalimbali katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

Jambo hilo limetoa fursa kwa wananchi kuwasikiliza na kuwapima wagombea wa vyama mbalimbali na litawasaidia kuchagua viongozi sahihi siku ya upigaji kura 

Hata hivyo amelitaka Jeshi la polisi kuendelea kusimamia amani katika kipindi chote cha uchaguzi ili watanzania waweze kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura katika hali ya utulivu na kuchagua viongozi bora.

“Sisi ka Tume yenye dhamana ya kusimamia haki na utawala bora tunaliomba jeshi la polisi linapotekeleza majukumu yake lizingatie maadili, kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kuepuka matumizi makubwa ya nguvu yasiyokuwa ya lazima”anasisitiza.

Mbali na hayo aliwasihi viongozi wa dini kuendelee kukemea maovu na kuliombea taifa katika kipindi hiki muhimu ili haki, amani, utulivu na upendo viendelee kudumishwa sasa na hata baada ya uchaguzi kumalizika.

Katika tamko hilo ,Mwaimu pia amewataka Wagombea watakaoshindwa katika kila ushindani ni lazima awepo mshindi na atakaeshindwa, na kwamba wagombea watakaoshindwa wanaombwa wakubali matokeo ili kudumisha amani ya nchi .

“Ambaye hataridhishwa na matokeo, ni vema akafuata mkondo wa sheria na kanuni zilizowekwa zinazoruhusu kudai haki badala ya kutafuta njia za mkato katika kudai haki ambazo matokeo yake yanaweza kuwa hasi,Tume inawatakia Watanzania wote Uchaguzi mwema Mungu ibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”anasema

Post a Comment

0 Comments