USAFI WA 'WIKIENDI' WAKIMBIZA MAGONJWA YA MILIPUKO DODOMA

 

 


📌NA RACHEL CHIBWETE

 

Dodoma. Zoezi la usafi wa mazingira linalofanywa na wakazi wa Jiji la Dodoma kila Jumamosi limefanikisha Jiji hilo kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu kwa miaka mitano mfululizo.

 Hayo yameelezwa na Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, Abdallah Mahia wakati akizungumza CPC Blog kuhusiana na Jiji hilo lilivyoweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kipindi kirefu.

Mahia amesema Ugonjwa wa mlipuko uliokuwa unalisumbua sana Jiji la Dodoma ni kipindupindu hasa wakati wa mvua na msimu wa matunda hasa maembe kwenye miezi ya Oktoba hadi Machi ya kila mwaka.

Lakini kutokana na usafi wa mazingira unaofanywa na wakazi wa Jiji la Dodoma kila jumamosi na ujenzi na matumizi ya vyoo bora tumefanikiwa kujiepusha na magonjwa ya mlipuko tangu mwaka 2015 hadi sasa.

“Mwaka 2018 tulipata wagonjwa wanne wa kipindupindu lakini hawakuwa wakazi wa Jiji la Dodoma, walikuwa ni wasafiri kutoka mikoa ya Singida, Morogoro na Dar es salaam ambapo walikuja kutibiwa kwenye vituo vyetu vya afya na baada ya kupona waliendelea na safari zao,” amefafanua Mahia.

Ameongea kuwa wakazi wa Dodoma wameelimika na wamekuwa wakiitumia vizuri siku ya jumamosi kwa ajili ya kufanya usafi kwenye makazi yao ambapo kwa kiasi kikubwa wameweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakiwasumbua kila mara.

Amesema pia kutokana na ujenzi wa vyoo bora wameweza kuwathibiti wale waliokuwa wakitapisha majitaka kwenye mitaro ya maji ya mvua ambayo yalikuwa yanasambaa kwenye makazi ya watu na kusababisha magonjwa ya kuhara na kutapika.

Pia amesema timu ya wataalam wa afya wamekuwa wakikagua mara kwa mara visima virefu na vifupi vinavyotumiwa na wakazi wa Jiji hili kwa ajili ya maji ya matumizi ya nyumbani kwa kuhakikisha kuwa maji hayo ni salama.

 Hata wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa corona tulitoa elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo ambapo wananchi wetu walituelewa na ndiyo maana mpaka sasa utaona kuwa hakuna takataka zozote za barakoa zinazozagaa mitaani kwa sababu tuliwafundisha namna ya kuzihifadhi na kuziteketeza

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya mazingira na udhibiti taka ngumu Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro amesema suala la usafi wa mazingira ni muhimu hivyo ni wajibu wa kila mtu kushiriki.

Amesema sheria ya kuwatoza faini kati ya Sh 50,0000 hadi 300,000 mtu atakayekamatwa anachafua mazingira kwa kutupa taka ovyo imesababisha mazingira ya Jiji hilo kuwa safi na kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.

Amesema kwenye maeneo mengine wanatumia vikundi vya wafanya usafi kukusanya taka zote za majumbani na kuzipekeleka kwenye dampo la Jiji lengo ni kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama.

 

Post a Comment

0 Comments