WAZIRI MWAKYEMBE:HALI YA UTOAJI WA TAARIFA KWA TAASISI ZA UMMA BADO IPO CHINI


Waziri wa Habari,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe
 akizindua 'Ripoti ya Utoaji wa Taarifa kwa taasisi za Umma.


📌NA MWANDISHI WETU 

AZIRI wa Habari ,Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe amesema pamoja na kuwepo kwa sheria ya Habari ,hali ya uwajibikaji wa utoaji Habari bado ipo chini katika taasisi za umma .

Dkt.Mwakyembe amebainisha hayo leo Oktoba 2,2020 jijini Dodoma katika maadhimisho ya siku ya haki ya kupata taarifa duniani  yaliyoandaliwa na Taasisi ya vyombo vya Habari kusini Mwa Afrika ,Tawi la Tanzania[MISA-TAN].

Dkt.Mwakyembe amesema pamekuwepo na changamoto kwa watumishi wa umma kutokuwa na ushirikiano wa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ili wananchi wajue kinachoendelea hali ambayo husababisha wananchi hao kushindwa kupata taarifa kwa usahihi na kusababisha malalamiko hivyo ni wajibu kwa kila mtumishi wa Umma kuwa na ushirikiano wa utoaji wa taarifa .

Pia ,Waziri Mwakyembe amesema kuna baadhi ya Watumishi wa umma wamekuwa hawapokei simu za waandishi wa Habari pindi wanapohitaji taarifa muhimu hali ambayo husababisha sheria ya  haki ya kupata taarifa kuvunjwa  jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utawala bora.

Unakuta mtumishi wa umma anapopigiwa simu na mwandishi wa habari hapokei hata simu na ukiangalia hata sababu za kutokupokea simu hazipo ni wajibu watumishi wa umma kutoa taarifa ili mwananchi ajue nini kinaendelea katika nchi yake.

Dkt.Mwakyembe

Hata hivyo,Waziri Mwakyembe ametumia fursa hiyo kuvipongeza vyombo vya habari na wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii  huku pia akipongeza taasisi za serikali zilizotunikiwa vyeti kwa ubingwa wa utoaji wa taarifa kwa wananchi.



Dkt.Mwakyembe akimkabidhi tuzo ya Golden Key Award kwa
Afisa Kumbukumbu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Japhet Baluyha.Katika Utafiti huo WCF iliibuka mshindi wa tuzo hiyo kwa kuwa wawazi katika kutoa taarifa kwa Umma.


Aidha ,suala la  uhaba wa Maafisa habari katika halmashauri limeibuka katika maadhimisho hayo ya siku ya kupata taarifa duniani  ambapo baadhi ya wajumbe wa MISA-TAN wametoa hoja ya kuwa na umuhimu kwa kila halmashauri kuwa na afisa habari kuliko kuingiliana majukumu na kitengo cha TEHAMA  hususan kwa wataalam wa ICT kufanya majukumu kama wanahabari.

Akijibu hoja hiyo,Waziri Mwakyembe amesema serikali ina mpango wa kuweka mfumo mzuri zaidi katika kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na Maafisa Habari.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Taasisi ya vyombo vya Habari kusini Mwa Afrika ,Tawi la Tanzania[MISA-TAN] Bi.Salome Kitomari amesema miongoni mwa shughuli ambazo zimekuwa zikifanywa na MISA-TAN ni pamoja na kufanya tafiti ambapo bado kuna usiri hata mambo ya kawaida kabisa  katika utoaji wa taarifa .

Utafiti ulibaini kuwa zipo ofisi za umma ambazo ukipiga simu saa za kazi haiwezi kupokelewa na wakati mwingine unaweza kudhani labda mhusika katoka kidogo.Lakini unapopiga simu mara kadhaa kwa nyakati na siku tofauti bila majibu,inatia shaka sana.

Salome Kitomari

Katika maadhimisho hayo,shirika la Mawasiliano Tanzania[TTCL]limepata tuzo ya Uminyaji  taarifa[Golden Padlock]kutoka Taasisi ya vyombo vya Habari kusini Mwa Afrika ,Tawi la Tanzania[MISA-TAN] .

 





Post a Comment

0 Comments