WIZARA YA AFYA YATAHADHARISHA JAMII MAGONJWA YA MLIPUKO



📌NA DOTTO KWILASA

 KUFUATIA kuanza kunyesha kwa mvua kubwa katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo Mkoa wa Dar Es Salaam,Wizaraya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa Wananchi kuhusu namna ya kujikinga na  kuepuka magonjwa ya mlipuko. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini hapa,Mganga Mkuu wa Serikali,Profesa Abel Makubi alisema kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha kuna uwezekano mkubwa kuibuka kwa  magonjwa ya milipuko  kama kuhara damu,Kipindupindu na yale yanayoenezwa na Mbu ambayo ni  Malaria na Dengue.

Kutokana na hayo,amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuendelea kushirikiana  kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa, wananchi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila eneo  haligeuki kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko.

Tumeshuhudia kuanza kujitokeza kwa uharibifu wa miundombinu ikiwemo ile ya kusafirisha  na kuhifadhia maji safi na taka ambapo hali hii itahatarisha  afya ya jamii na hivyo kuongeza uwezekano  wa kusababisha kuenea kwa urahisi kwa magonjwa ya kuambukiza na yale ya mlipuko

Licha ya hayo Mganga Mkuu huyo  alizitaja kanuni na taratibu za kiafya zinazotakiwa kufuatwa na wananchi ni pamoja na  kuchemsha maji ya kunywa,kuepuka kula  chakula kilichopoa,au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.

Prof.Makubi alizitaja kanuni zingine ni kutumia ipasavyo vyoo na kunawa mikono kwa maji safi na maji tiririka na sabuni kabla ya kula,baada ya kutoka chooni,baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia na baada ya kumhudumia mgonjwa.

Kanuni nyingine ni  kuosha matunda na maji safi kabla ya kula,kuongeza usimamizi wa usafi wa jumla na mikono  katika maeneo ya mikusanyiko kama shuleni,vyuoni na masokoni.

Pamoja na mambo mengine Mganga Mkuu huyo wa Serikali alizitaja sababu zingine ni kutotapisha vyoo,kujikinga kuumwa na mbu pamoja na kutumia vyandarua,kusimamia hali ya usafi  katika mifumo ya maji safi,maji taka na mitaro.

“Kwa hiyo nawaomba sana waganga wetu wa wilaya wachukue tahadhari katika hili  mtafute namna ya kuweza kushirikiana na mamlaka ndani ya kila eneo ili kuzuia maambukizi,amesema na kupongeza;

Wizara tutaendelea kuwakumbusha tiba ni bora kuliko kinga.

Katika hatua nyingine Prof.Makubi aliitaka jamii kuendelea kumuenzi baba wa Taifa Julius Nyerere kwa kuendeleza juhudi na mafanikio katika kudhibiti magonjwa kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele kusimamia kupingana na maadui watatu ikiwemo maradhi.

 


Post a Comment

0 Comments