📌BEN BAGO/MTANDAO
UKOSEFU wa vyoo bora katika jamii nyingi duniani umebainishwa kama mojawapo wa sababu inayochangia kwa kiasi kikubwa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.
Hivyo basi serikali nyingi duniani hususani nchi za dunia ya tatu ambako tatizo linaonekana kuwa kubwa zaidi, zinapambana kuondokana na tatizo.
Kwa mujibu wa Shirika la
Afya Duniani (WHO) zaidi ya watu bilioni 20 duniani inasemekana hawana
vyoo. Kati yao watu milioni 673 wanajisaidia kwenye maeneo ya wazi ikiwemo
vichakana, vichochoroni na hata kwenye vyanzo vya maji hali inayosababisha asilimia
10 ya watu dunia kutumia mboga mboga zilizomwagiliwa na maji machafu.
Kwa upande wa Tanzania,
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa takwimu zinaonyesha
watu wapatao 30,000 huugua magonjwa ya kuhara kila mwaka na baadhi yao hupoteza
maisha, hivyo jamii inatakiwa kuzingatia usafi wa mazingira ili kuepuka
vifo hivyo ambavyo inakadiriwa ni sawa na idadi ya wastani wa watu 83 kwa siku.
“Kama Taifa hatuna budi
kuwekeza nguvu na rasilimali zetu katika suala la usafi wa mazingira ikiwemo
matumizi ya maji safi na vyoo bora ili kufikia malengo yetu ya kitaifa pamoja
na yale ya kidunia,” amekaririwa Mhe. Samia Suluhu, wakati wa uzinduzi wa
kampeni ya nyumba ni choo, Disemba 8 jijini Dodoma.
Uhamasishaji wa ujenzi na
matumizi ya vyoo bora ili kuzuia magonjwa ya mlipuko ulianza rasmi
mwaka 1973 hadi mwaka 1978 ambapo serikali ilianzia kampeni iliyojulikana
kama “Mtu ni Afya.”
Kampei hii ililenga
kuhamasisha wananchi kujenga aina yeyote ile ya choo ili kuepuka mlipuko wa
magonjwa kama vile kipindupindu.
“Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli ameonyesha kusikitishwa kwake kutokana
na uwepo wa kipindupindu nchini, hivyo Watanzania hatuna budi kuwa wasafi wa
mazingira ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa huo,” alikaririwa aliyekuwa Waziri wa
Afya, Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya nyumba ni choo.
Wakati hali
yauboreshaji, ujenzi na matumizi ya vyoo ukiendelea kuwa katika viwango vya
juu, hali ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara yanapungua kwa
kasi.
Takwimu za kitaifa zinaonyesha
wazi kwamba uboreshaji wa usafi wa mazingira ukiwemo vyoo bora na matumizi
sahihi, upunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mlipuko.
Mkoa wa Dodoma unaweza
kuwa kielelezo katika eneo hili ambapo umiliki wa vyoo upo kwa asilimia 65.9
hali inayofanya mkoa huu kutopata kesi ya kipindupindu kwa takribana miaka
minne.
Katika kampeni ya nyumba ni choo iliyokuwa inaratibiwa na Wizara ya afya, Mkoa wa Dodoma imeshika nafasi ya tatu, hivyo tunajitahidi kuhamasisha matumizi bora ili tuendelee kuepuka magonjwa ya milipuko
Fransis Bukulu, Kaimu Ofisa Afya na Usafi wa
Mazingira Mkoa wa Dodoma.
SABABU ZINAZOWAFANYA WATU KUTOJENGA NA KUTUMIA VYOO
Zipo sababu kadhaa zinazoanishwa na watafiti kama ndio chanzo cha baadhi ya watu kutoona umuhimu wa kujenga na kutumia choo. Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa elimu ya afya ya mazingira pamoja na tabia ya mazoea.
Yapo mazoea kwa baadhi ya jamii kutojenga na kutumia vyoo
kutokana na mazoea waliyoyakuta katika jamii zao.
Mfano baadhi ya jamii zilizopo kandokando ya vyanzo vya maji
kama vile maziwa, mito na hata bahari, kujisaidia haja zote kwenye vyanzo
husika, hivyo vizazi vyao pia vinaendela na utamaduni huo ambao huchochea
magonjwa ya mlipuko.
Kwa mantiki hiyo, elimu na uhamasishaji wa ujenzi na matumizo
bora ya vyoo inahitajika katika maeneo hayo ikiwemo Mkoa wa Mara ambao katika
ripoti ya kampeni ya uhamasishaji wa ujenzi na matumizi ya vyoo “Nyumba ni
Choo” inaonesha mkoa huo unashika mkia.
TAHADHARI KATIKA MATUMIZI YA VYOO
Suala la ujenzi ni jambo la kuzingatiwa ambapo wataalamu wa afya wanasema
ujenzi usiozingatia mipango miji, unaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko
katika makazi ya watu.
Mara kadhaa hususani
maeneo ya mjini kumekuwa na malalamiko ya matumizi yanayokwenda kinyume na
kanuni za afya kutokana na utunzaji mbaya wa vyoo.
Mfano katika matumizi ya
vyoo vya maji, vyoo vinavyotumia maji kuna utaratibu zake ambao mhusika lazima
azifuate ili kulinda afya yake na majirani wanaomzunguka.
Vyoo vinavyotumia maji
husafirisha majitaka yenye kinyesi kupitia mifumo maalum ya bomba ambayo
hutengenezwa kwa ajili ya kazi hiyo. Husaidia kuboresha afya hasa katika maeneo
yenye msongamano wa makazi mijini na mara nyingi ndio aina ya vyoo ambavyo watu
wengi hupendelea.
Hata hivyo, gharama ya
kunyonya vyoo vinapo jaa huwa ni kubwa, hivyo mara nyingi huwalazimisha wenye
nyumba kuelekezea majitaka yenye kinyesi kwenye mito, maziwa au bahari.
Kuna watu wanakwepa gharama kunyonya maji yale kwa kutumia magari maalumu, kipindi cha mvua wanakitumia kutitirisha maji taka hayo kwenye mifereji ya maji ya mvua kitu ambacho ni hatari zaidi katika uthibiti wa magonjwa ya milipuko anabainisha
Abdalla Mahia, Afisa Afya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Afisa hiyo ameongeza kuwa hali hiyo hueneza
vijidudu vya maradhi kutoka kwenye majitaka hadi kwenye njia za maji
za kawaida au za majirani.
0 Comments