FAHAMU AINA YA NGO'MBE WENYE UWEZO WA KUTOA MAZIWA MARA NNE YA WALE WA ASILI.

 


📌Na Saleh Ramadhan.

 Taasisi ya Taifa ya utafiti wa mifugo kituo cha mpwapwa (TALIRI) imebainisha kuwa ng'ombe aina ya mpwapwa wanauwezo wa kutoa maziwa lita 5 mpaka lita 10 katika mazingira ya mfugaji ambayo ni zaidi ya Mara 4 ya maziwa anayotoa ng'ombe wa Asili.

 Hayo yamebainishwa Leo wilayani mpwapwa jijini Dodoma na Kaimu mkurugenzi Taasisi ya Taifa ya utafiti wa mifugo kituo cha mpwapwa (TALIRI) Dr.Aluna chawala ambapo amesema kuwa ulishaji wa mchanganyiko mzuri wa mikunde miti huongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa maziwa na nyama. 

"Ng'ombe aina ya mpwapwa ni Tunu ya Taifa  maana ng'ombe huyu ni matokeo ya utafiti uliolenga kuzalisha ng'ombe chotara kwa ajili ya nyama na maziwa kwa wingi katika mazingira kame" amesema Dr. Aluna chawala.

 Aidha,Dr Aluna chawala amesema kuwa ng'ombe aina chotara mpwapwa itaweza kuzalisha lita 3000 kwa kipindi cha ukamuaji wake mmoja ambayo ni wastani wa lita 10 hadi 16 kwa siku kutegemea na atakavyotunzwa.

 Kwa upande wake Deogratius Masao Mtafiti idara ya ng'ombe amesema kuwa Teknolojia ya kuzalisha ng'ombe chotara ni kuboresha mifugo Asili na kuwajengea wafugaji mazingira bora ili wajipatie kipato kizuri kupitia Teknolojia hii.

"Halmashauri zote zenye wafugaji wengi zikifanya utaratibu wa kufikisha elimu ya teknolojia hii ngazi ya kijiji mpaka kata itawafanya wafugaji wavutiwe na ufugaji huu". Amesema Deogratius masao.

Naye Mtafiti idara ya mbuzi Boniface paschal amebainisha kuwa mbuzi aina ya malya au Blended ni mbuzi aliyetokana na utafiti uliokusudia kuzalisha mbuzi anayefaa kwa nyama na maziwa.

" utafiti huu wa mbuzi aina ya malya ni kumuongezea lishe na kipato mfugaji, mbuzi huyu ni mchanganyiko wa mbuzi Asili-kamorai kutoka pakistani na Boer kutoka Africa Kusini, pia wanauwezo wa kuzaa watoto mapacha au watatu na wanauwezo wa kuzaa hadi Mara 3 katika kipindi cha miaka miwili" amesema 

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya sayansi na Teknolojia (COSTECH) imetumia Billion 50 katika kufadhili Miradi ya utafiti na ubunifu nchini ambapo Miradi zaidi ya 100 imefadhiliwa na Asilimia 70% imekamilika.

 

Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments