HATUA ZA KUZINGATIA UNYONYESHAJI MTOTO KWA MAMA MWENYE CORONA

  


📌MUSSA YUSUPH

MEI mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mtandao wa Kimataifa kuhusu Chakula cha Mtoto (IBFAN), yalitoa tafiti yakieleza dhana potofu kuhusu maziwa ya mama kwamba yanaweza kusababisha maambukizi ya virusi vya Corona kwa mtoto.

Katika utafiti huo, mashirika hayo yamehamaisha wakina mama waendelee kunyonyesha mtoto, hata kama amethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anashukiwa kuwa navyo.

 Kupitia utafiti huo mashirika hayo yameeleza: “Wakati watafiti wanaendelea kuchunguza maziwa kutoka kwa mama mwenye virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona, ushahidi wa sasa unadokeza kuwa hakuna uwezekano wa virusi hivyo kuambukizwa kupitia unyonyesaji au kwa kumpatia mtoto maziwa yaliyokamuliwa kutoka kwa mama mwenye virusi au anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona.”

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa (UN) unaeleza kuwa uchunguzi kutoka mataifa 194, umebaini kuwa ni nchi sita pekee ambazo zina mikakati ya kisheria kuhusiana na kanuni ya kimataifa ya kutangaza maziwa mbadala ya mama.

Kanuni hiyo inapiga marufuku aina zote za matangazo ya maziwa mbadala ya mama, ikiwemo matangazo, zawadi kwa wahudumu wa afya na mgao wa bure wa sampuli za maziwa hayo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Dkt. Francesco Branca, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula kutoka WHO, amesema kuwa, “Mikakati mizito ya matangazo ya maziwa ya unga kwa mtoto, hasa kupitia wataalam wa afya ya kwamba wazazi waamini ushauri wa lishe na afya, ni pigo kubwa katika kuimarisha afya ya mtoto.”

WHO na UNICEF wanapendekeza kuwa mtoto anyonye maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya mwanzo na baada ya hapo aendelee kunyonya hadi miaka miwili na zaidi huku akipatiwa vyakula vingine vyenye lishe.

Mkuu wa masuala ya lishe UNICEF, Dk. Victor Aguayo, amesema kuwa kadri janga la COVID-19 linavyozidi kuenea, wahudumu wa afya wanaelekezwa maeneo ya kusaidia kudhibiti janga hilo, huku suala la unyonyeshaji ambalo linaokoa maisha ya mamilioni ya watoto, linakosa mwongozo wa kutosha.

Tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kila mama na kila familia inapata mwongozo unaotakiwa kutoka kwa wahudumu wa afya waliobobea ili waweze kunyonyesha watoto wao tangu wanapozaliwa.

HATUA ANAZOPASWA KUZINGATIA MAMA WENYE CORONA

Utafiti huo wa UN, unaeleza kuwa mama aliyethibitishwa kuwa na virusi vya Corona au anayeshukiwa kuwa na virusi hivyo, anaweza kuendelea kunyonyesha na kwamba anapaswa kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji safi na sabuni au dawa za kutakasa mikono kabla ya kumbeba au kumshika mtoto.

Pili anapaswa avae barakoa ya kitabibu wakati akiwa amembeba au anamhudumia mtoto ikiwemo wakati anamlisha.

Tatu, apigie chafya au akoholee kwenye kitambaa kisha anawe mikono na nne, asafishe eneo mara tu anapokuwa ameligusa.

Akizungumzia kuhusu huduma za lishe kwa mama mjamzito na anayenyonyesha mwenye maambukizi ya COVID -19, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Fatma Mwasola, anasema kanuni za lishe ya mama mjamzito na anayenyonyesha zifuatwe ikiwa ni pamoja na kula mlo kamili unaotokana na vyakula mchanganyiko mara nne mpaka tano na asusa mara mbili kwa siku.

Ili kupata unasihi wa kunyonyesha, anasema msaada wa msingi wa kisaikolojia na kijamii na msaada wa ulishaji unaostahili utolewe kwa akina mama wajawazito na wenye watoto wachanga na wadogo, bila kujali wao au watoto wao wachanga na wadogo wanahisiwa au wameambukizwa COVID-19.

Fatma anaeleza pia, wakina mama hao muhimu wapatiwe huduma za kujikinga na athari za COVID ili wasiambukizwe au wasiwaambukize wengine kwa kujitenga na mwingiliano na kuchukua hatua nyingine zinazoweza kusambaza maambukizi.

Washauriwe kupata huduma za kliniki na kusaidiwa pale wanapokutwa na matatizo mbalimbali.

UMUHIMU WA UNYONYESHAJI WATOTO WAKATI WA CORONA

Ofisa Mtafiti huyo wa masuala ya lishe anaeleza kuwa kunyonyesha mtoto huzuia vifo pamoja na magonjwa mara baada ya mtoto kuzaliwa na wakati mtoto akiwa mchanga na mdogo.

Anasema matokeo ya kumkinga mtoto ni makubwa kupitia uimarishaji wa kingamwili moja kwa moja toka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hivyo, anaeleza kuwa kanuni zinazoshauriwa katika ulishaji wa watoto wachanga unaokubalika ni muhimu kuzingatiwa pamoja na kuchukua tahadhali za kuzuia maambukizi ya COVID 19.

“Watoto waliozaliwa na wanawake wenye maambukizi ya Corona walishwe kwa kuzingatia mwongozo wa kitaifa wa ulishaji watoto wachanga na wadogo, na mama zao wazingatie taratibu zinazopendekezwa za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

“Anza kunyonyesha mtoto mapema katika kipindi cha ndani ya saa moja baada ya kujifungua. Mnyonyeshe mtoto maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na mtoto akitimiza umri wa miezi sita anza kumpa vyakula vya nyongeza na endelea kumnyonyesha maziwa ya mama hadi atimize umri wa miaka miwili au zaidi,” anabainisha.

Mtaalamu huyo anaeleza kama inavyofanyika kwa watu walioambukizwa virusi vya Corona, wanawake wanaonyonyesha wanaotekeleza taratibu ya kugusana na watoto wao kimwili au ubebaji watoto kwa mtindo wa kangaroo, wanapaswa pia kuzingatia taratibu za usafi wa mwili na kuzuia majimaji yanayotoka puani na kwenye mfumo wa kupumua wakati wote wanapowanyonyesha watoto wao.

“Kwa mfano wanapaswa kutumia vifaa vya kufunika pua na mdomo unapokuwa karibu na mtoto, kunawa mikono mara kwa mara kabla na baada ya kumhudumia mtoto, kusafisha na kutakasa maeneo yote ambayo mama mwenye maambukizi ameyagusa.

Anaongeza kuwa: “Wanawake wajawazito na wanawake wenye watoto wachanga na wadogo wapate ushauri nasaha kuhusu unyonyeshaji, ulishaji watoto na huduma za msaada wa kisaikolojia iwapo wao wenyewe au watoto wao wanahisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mtaalamu huyo anaeleza: “Inapotokea kuwa mama mwenye maambukizi makali ya virusi vya Corona au matatizo mengine ya kiafya yanayosababisha ashindwe kuendelea kumnyonyesha mtoto wake, ashauriwe na asaidiwe kukamua maziwa yake, na kumlisha mtoto maziwa hayo yaliyokamuliwa. Hayo yafanyike sanjari na kuzingatia taratibu zinazoshauriwa za kudhibiti maambukizi.”

Fatma anaeleza kuwa mama na mtoto wasaidiwe kugusana mwili, kubeba mtoto kwa mtindo wa kangaroo, kukaa pamoja bila kutenganishwa mchana na usiku, hasa mara baada ya mama kujifungua na siku za mwanzo wakati mama anapoanzisha unyonyeshaji, bila kujali iwapo mama au mtoto anahisiwa au amethibitiishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.

Anaeleza kuwa wazazi na walezi wanaohitaji kujitenga au kutenganishwa na watoto wao, na watoto wanaohitaji kujitenga au kutenganishwa na wazazi au walezi wao, wanapashwa kupata huduma saidizi za kitaalamu kutoka kwa watoa huduma za afya, au watoa huduma wengine wa afya ya akili na msaada wa kisaikolojia

Post a Comment

0 Comments