MAFUNDI UJENZI KUWENI NA UMOJA ILI KUTAMBULIKA KWA LENGO LA KUNUFAIKA NA FURSA ZA UJENZI.

 


📌NAZA KIRIMBO.

MBUNGE  wa jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ametoa wito kwa mafundi ujenzi kuwa na umoja ili kutambulika kwa lengo la kunufaika na fursa za ujenzi zilizopo jijini hapa.

Mavunde aliyasema hayo jijini hapa katika halfa iliyoandaliwa Kampuni uzaji wa vifaa vya ujenzi ya Najel Builders na kuwakutanisha mafundi ujenzi zaidi ya 50.

Alisema kupitia umoja huo itasaidia kundi hilo kuunganishwa na fursa za ujenzi zinazopatikana jijini hapa ili kunufaika na uwepo wa Makao Makuu ya nchi, Dodoma.

Mathalan,alisema baada ya kujiunga au kuunda umoja huo, utawanufaisha, kwanza kwa kuwa na anwani lakini pia kupata fursa mbalimbali za kutoa huduma ya ujenzi.

“Mkiwa na umoja wenu, zinapotokea kazi inakuwa rahisi kuwaunganisha, unawaambia tu kuwa nenda sehemu mflani utapata mafundi wazuri, waaminifu ambao watafanyaka kazi nzuri. Hii itasaidia hata mmoja wenu akifanya jambo la tofauti awe anapoteza sifa ili asiwachafue wengine,” alisema Mavunde.

Mavunde alisema pamoja na kuwa na mafundi wengi jijini hapa,kikubwa ni uaminifu ambayo ni silaha ya mafanikio.

Alisema wapo watu hawana mtaji wa fedha lakini wana mtaji wa uaminifu hivyo kupitia uaminifu huo wamekuwa wakipata kazi nyingi.

Hata hivyo alisema kupitia umoja huo atawasaidia mafundi hao kupata bima ya afya ili kuwa na uhakikia wa matibabu.

“Kwa kazi ambazo mnazifanya ni lazima muwe na bima ya afya, ni lazima tuilinde nguvu kazi yetu. Na katika hili siku yeyote mkiwa tayari niambieni nitawatafutia mtaalam aje awaelimishe kuhusu masuala ya bima ya afya sanjari na umuhimu wake,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi mtendaji ya Kampuni ya Najel Builders Neema Nzwalile alisema kutokana na changamoto ya wajenzi wengi Dodoma kukosa mafundi na ushauri wa kitaalamu kampuni hiyo iliamua kutafuta suluhisho la tatizo hilo.

Nzwalile alisema waliamua kumrahisishia mjenzi kupata vifaa na mafundi pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya ujenzi.

Alisema Dodoma inakua kwa kasi na katika ukua huo inahitaji mafundi ambao wanafanya kazi vizuri ambapo ili kufikia lengo hilo wameamua kuwakutanisha mafundi kwa lengo la kuunda umoja wao.

Alisema lengo ni kuwaunganisha mafundi wote ili wanufaike na fursa zilizopo jijini hapa.

Naye mwenyekiti wa mafundi hao Wille Sakalani alitoa shukrani kwa ahadi zilizotolewa na mbunge huku akisema  malengo yao ni kufikia hatua ya kusajili kikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ikiwamo mikopo.

Mwisho.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments