📌RONALD SONYO
KWA mujibu wa takwimu za Umoja
wa Mataifa (UN) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu bilioni moja wanaishi kwenye
makazi holela huku ikitarajiwa idadi hiyo kuongezeka mara mbili zaidi ifikapo mwaka
2030.
Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia makazi (UN-HABITAT) limefafanua kuwa makazi duni au holela
ni eneo la miji lenye ukosefu wa huduma za msingi (usafi wa mazingira, maji ya
kunywa, umeme) na lenye msongamano wa nyumba na watu.
Tafiti mbalimbali
zinaonesha hali hiyo inasababishwa na ongezeko la watu mijini, kupanuka kwa
mipaka ya miji, kukosekana kwa ardhi huru iliyopangwa, uwezo mdogo kiuchumi wa
mamlaka za upangaji na kukosekana kwa nyumba zenye gharama nafuu.
Takwimu zinaonesha kwamba,
Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 71.8 ya wakazi wa mijini kuishi katika
makazi yasiyo rasmi.
Kwa upande wa Tanzania, kwa
mujibu wa Ripoti ya Miji Tanzania iliyoandaliwa na Mtandao wa Miji Nchini ya
mwaka 2014, wastani wa kiwango cha ujenzi holela kwenye miji hiyo ni asilimia
67.
Aidha, wananchi wengi
kutozingatia Sheria ya Mipangomiji, upungufu wa rasilimali watu na fedha pamoja
na kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika kusimamia Sheria za Mipangomiji ni
miongoni mwa sababu za ongezeko hilo.
MAKAZI HOLELA NA MAGONJWA YA MILIPUKO
Makazi yaliyojengwa
kiholela yamekuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa na magonjwa ya milipuko
kutokana na sababu mbalimbali.
Moja ya sifa ya makazi
holela ni hali ya kutopatikana kwa huduma za kijamii kama vile maji hali ambayo
inasababisha kwa kiasi kikubwa mlipuko wa magonjwa.
“Mengi ya maeneo
hayo hayana miundombinu na huduma za msingi kama vile maji safi na salama,
barabara na mifereji ya maji ya mvua na udhibiti wa majitaka na taka ngumu,” alikaririwa
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, katika
Bunge la 11 alipokuwa akijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo
Peneza (Chadema).
Dk. Mabula amesema hali
hiyo husababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa, mazalia ya mbu, nzi na
mandhari mbaya ya kuishi inayosababisha afya duni na kupunguza nguvukazi.
Pia mengi ya maeneo hayo
hayana miundombinu na huduma za msingi kama maji safi na salama, barabara, mifereji
ya maji ya mvua na udhibiti wa majitaka na taka ngumu.
Zote hizi ni athari mbaya
kwa kuwa mafuriko yamekuwa yakitokea katika makazi mengi ya mijini kutokana na
ujenzi holela, mazalia ya mbu na inzi nayo ni chimbuko la malaria na magonjwa
ya milipuko.
MSONGAMANO
Maeneo haya yanabainishwa
kuwa hatari zaidi katika usambaaji na uambukizwaji wa magonjwa ya mlipuko
ikiwemo COVID-19.
Msongomano wa watu katika
makazi holela inawafanya wakazi wa maeneo haya kutoweza kuzingatia ushauri wa
wataalamu wa afya unaotaka watu kukaa umbali wa mita kadhaa ili kupunguza
maambukizi.
Kwa mujibu wa Shirika la
Afya Duniani (WHO) jamii zinazoishi kwenye hali msongamano zipo kwenye hatari
zaidi ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Katika makazi yenye
msongamano wa watu ni hatari zaidi katika maambukizi ya magonjwa yenye uwezo wa
kuambukizana kama vile maambukizo ya vikoozi, TB na magonjwa mengine ya
upumiaji, kipindupindu na magonjwa ya ngozi ikiwemo upele.
Hali ya hatari pia ipo
katika miundombinu mingine ya umma kama vile vituo vya afya ambako mara nyingi
vimeonekana kuwa na uwezo mdogo kuliko idadi ya watu inayojitokeza kufuata
huduma katika vituo hivyo.
Msongamano wa watu
hurahisha usafirishaji wa viini (germs) kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine.
Katika maeneo ya masoko
na vituo vya mabasi nako kuna hatari zaidi ya kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.
“Ni kweli kama hakuna
mipangilio mzuri wa miji magonjwa ya milipuko lazima yajitokeze mara kwa mara
lakini kama miji imepangika vizuri hatari inakuwa haipo kwa vile hata mitaro ya
maji taka itaeleweka, barabara zitakuwepo na hata vyoo vikijaa inakuwa rahisi
kuvi-empty (kunyonya kinyesi),” anaeleza, Fransic Bukulu, Ofisa Afya na Usafi
wa Mazingira Mkoa wa Dodoma.
NINI KIFANYIKE?
Kwa kuona umuhimu wa
kupambana na janga la makazi holela serikali ilianzisha Programu ya kitaifa ya
kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini ya mwaka 2015-2025
inayolenga pamoja na mambo mengine kuzuia na kudhibiti ujenzi holela ambao
husababisha kuwepo kwa makazi duni, hivyo utekelezaji wa mpango huo uwe
endelevu ili kutokomeza makazi holela nchini.
Pia mamlaka husika
(zikiwemo Mamlaka za Maji Safi na Taka na usafi wa Mazingira) zijitahidi
kupeleka huduma kijamii ili kupunguza madhara yatokanyo na ukosefu au upungufu
wa huduma hizo.
Wananchi wapewe elimu ya
madhara ya kuishi kwenye makazi holela na elimu ya usafi wa mazingira katika
maeneo hayo ili kujilinda na magonjwa.
0 Comments