WANAWAKE WAMETAKIWA KUPAZA SAUTI JUU YA UKATILI WANAOFANYIWA NA WEZA WAO


 


📌NA HAMIDA RAMADHANI DODOMA


MATUKIO ya wanawake kutotoa taarifa na kupaza sauti zao juu ya ukatili wanaofanyiwa na wenza wao yamekithiri nchini na jambo kubwa likisadikika ni kuhofia kukosa matunzo ya kifamilia.

Hayo yameelezwa leo jijini hapa na Reuben Charles kutoka Peace Relief Organization (PRO) kutoka Sumbawanga alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika kikao cha kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya harakati za kupinga ukatili wa kijinsia kikao kilichoandaliwa na  TGNP Mtandao kwa udhamini wa FCs Taasisi ya asasi ya kiraia.

Reuben kutoka Peace Relief Organization (PRO) Sumbawanga amesema wanawake kuogopa kuwaripoti waume zao au wapenzi wao kunachangiwa na elimu ndogo hali inayopelekea wanawake wengi kupoteza maisha huku wengine wakipata ulemavu wa maisha.

Hapa tunaona tatizo kubwa ni elimu wanawake wengi wanaogopa kutoa taarifa za ukatili wanaoupata  katika nyumba zao kwa kigezo cha kuhofia kukosa matunzo pindi wenza wao wanapotiwa mikononi mwa Sheria lakini  tuseme wazi anayetakiwa kupaza sauti ni mwanamke mwenyewe, amesema Charles.

Na kuongeza kusema kuwa "Endapo ikatokea Wanawake wote wanaofanyiwa ukatili wanasema au mmoja akajitokeza na kusema ukatili anaofanyiwa na mwenza wake hakika italeta hamasa kwa wengine kusema ukatili wanaofanyiwa majumbani mwao," amesema.

Aidha amewatoa hofu wanawake kwa kueleza kwamba si kila kesi za ukatili zinazolipitiwa mwanaume anaishia kufungwa jela hapana kesi zingine zinasuruhishwa na faida ni kwamba vitendo hivyo vya ukatili kupungua na kuisha kabisa kwa baadhi ya familia zilizowahi kuwa na migogoro.

Naye Tatu Mroto Mwanasheria kutoka Action For Justice In Society (AJISO) Mkoani Kirimanjaro amesema tatizo kubwa ni uelewa wa Sheria katika jamii, kwani ni mdogo kutokana na lugha inayotumika katika sheria zilizochapishwa.

Sheria zirahisishwe na ziwekwe katika lugha ya kiswahili ili iwe rahisi kwa jamii kuzisoma  na kuzielewa zaidi, amesema Mwanasheria Tatu.

Kwa upande wake Mwanasheria kutoka TGNP Mtandao Consolata Chikoti amesema kuwa kwasasa hali ni nzuri kutokana na Serikali kupitisha na kuzitaka mahakama zote kumaliza kesi mapema na kesi zote zisizidi miezi sita.

Hata hivyo amesema huko nyuma hali ilikuwa mbaya kutokana na kesi kuchukua muda mrefu hali iliyokuwa inapelekea kunyimwa haki ya mtu na ushahidi kupotea kabisa na baadhi ya watuhumiwa kukimbia kabla ya kesi kuisha.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments