WANAWAKE WANAKWAMISHA KESI ZA UKATILI WA KIJINSIA



  ðŸ“ŒRACHEL CHIBWETE

WAKATI dunia ikiwa kwenye maashimisho ya siku 16 za kupinga ukatili, umeelezwa kuwa wanawake bado wanakwamisha kesi za ukatili kwa kuwaficha wanaume wanaowafanyia ukatili kwa kuwa ndiyo wanaowategemea kiuchumi.

Hayo yamebainishwa kwenye kikao cha asasi za kiraia zinazojishughulisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia kilichofanyika Jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye kikao hicho cha tathmini Mratibu wa mradi huo kutoka Mtandao wa Kijinsia (TGNP) Zainabu Mmari  amesema Kuna kila sababu sasa ya wanawake na wasichana kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuwafichua wanaume wanaowafanyia ukatili huo wa kijinsia.

Hapa inaonekana kuwa changamoto inayowakabili watu wengi ni baadhi ya wanawake kuwaficha wanaume wanaowafanyia ukatili wa kijinsia kwa kuwa hao hao wanaume ndiyo wanaowapa mkate wao wa kila siku na hivyo kushindwa kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria.
Zainabu Mmari

Ameongeza kuwa, "Ili Sasa wanawake hao waamke na kupaza sauti zao pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili ni lazima  wawe na shughuli zinazowaingizia kipato hiyo itasaidia kuwaripoti kwenye vyombo vya sheria wanaume wanaowafanyia ukatili wa kijinsia."



Amesema vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia hufanyika kwa wanawake na watoto lakini baadhi yao hulazimika kukaa kimya kwa sababu wanaowafanyia ukatili huo ni waume zao hivyo wakishikiliwa na vyombo vya sheria  watabaki wanateseka na watoto wao.

Kwa upande wake mratibu wa miradi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Peace Relief Organization (PRO) Reuben Charles alisema wanawake wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili na waume zao lakini wanaogopa kuwaripoti kwa kuhofia kuachika kwenye ndoa zao.

Charles amesema siyo kila kesi ya ukatili wa kijinsia huishia kwa mtuhumiwa kufungwa bali kunaweza kutokea suluhisho la kudumu kupitia vyombo vya sheria bila mtuhumiwa kuhukumiwa kifungo gerezani.

Amesema ni wakati sasa wa kuwajengea wanawake uwezo wa kisheria ili wajue haki zao hasa pale wanapokutana na unyanyasaji wa kijinsia ili wajue mahali pa kupata haki zao kisheria.

Naye Mwanasheria wa TGNP Consolata Chikoti amesema endapo kesi za ukatili wa kijinsia zitaripotiwa na kutatuliwa kwa wakati zinasaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kupata haki yao kwa wakati.

Amesema madhara ya kuchelewesha kesi hizo ni pamoja na kupoteza ushahidi muhimu dhidi ya watuhumiwa na kutoa nafasi kwa watuhumiwa au ndugu zao kutoa vitisho vya waathirika wa vitendo vya ukatili na hivyo kusababisha kufuta kesi mahakamani au kutotokea kwenye kesi

Post a Comment

0 Comments