KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAANZA KAZI RASMI.

 


📌TITO MSELEM.

 MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula ameongoza ufunguzi wa Kikao cha Kwanza cha Kamati hiyo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 kilichofanyika leo Januari 25, 2021,  jijini Dodoma ili kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini.

Katika kikao hicho, Kitandula amempongeza Waziri wa Madini Doto Biteko kwa kazi nzuri inayofanywa katika kusimamia na kuiongoza Sekta ya Madini ikiwemo na kufanikisha upatikanaji wa Ithibati ya Cheti cha Uhalisia kwa Madini ya Bati.

Imeelezwa kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo, vya ununuzi wa madini, umechangia kuondoa changamoto ya ukosefu wa mahali pakufanyia biashara ya madini hususan kwa wachimbaji wadogo na hivyo kuwahakikishia bei stahiki na usalama.

Waziri wa Madini Doto Biteko, ameileza Kamati hiyo kuwa, uanzishwaji wa masoko ya madini umepelekea udhibiti wa utoroshaji wa madini ambapo masoko hayo yameleta manufaa kwa wananchi ikiwemo kuzalisha fursa za ajira na kuongezeka kwa kipato cha wachimbaji wadogo tofauti na ilivyokuwa awali.

Akijibu swali la Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Msalala Iddi Kassim Iddi, Waziri Biteko amesema, Wizara ya Madini imeimarisha udhibiti na usimamizi wa uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini ili kufaidisha Taifa na wawekezaji kwa usawa ambapo Wizara kupitia Tume ya Madini imeweka Msimamizi kila mgodi mkubwa ili kusimamia uzalishaji wa kila siku na kuepusha udanganyifu.

“Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo au kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za msingi za kijiolojia, kutoa huduma za kijiolojia kwa gharama nafuu, kuwawezesha wachimbaji wadogo kuwa wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa na pia kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo”, alisema Waziri Biteko.

Waziri Biteko ameongeza kuwa, wapo baadhi ya wamiliki wa mashamba katika maeneo mbalimbali ambapo madini yanagunduliwa na  hawafahamu haki ya ardhi na haki ya leseni ya madini . 

"Wao  wanadhani ukiwa unamiliki ardhi ya juu na madini yaliyopo chini ni ya mwenyeshamba, kitu ambacho si kweli, hivyo kuleta changamoto kubwa katika maeneo,'' amesema Waziri Biteko.

Ameongeza kuwa, wizara inalojukumu la kuwaelimisha na kuwashauri wenye mashamba kuungana na mwenye leseni ili wachimbe kwa pamoja.

Akijibu swali la Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu, Prof. Shukrani Manya, amesema mchimbaji mdogo wa madini anatakiwa kwenda kuuza madini yake kwa dalali (Brokers) na dalali atauza madini hayo kwa Mnunuzi mkubwa (Dealer). 

Ameeleza kuwa, haipaswi  kwa mchimbaji mdogo kumvuka  dalali na kwenda kuuza madini yake kwa Mnunuzi mkubwa (Dealer) moja kwa moja.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof Simon Msanjila, akijibu swali la msingi kutoka kwa Iddi Kassim Iddi Mbunge wa Msalala kuhusu Mpango wa Wizara kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, amesema kuwa, Wizara ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa wadau wote wa madini hususan wachimbaji wadogo pamoja na watumishi ya wizara hiyo ili kuepuka maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi.  

Akiwasilisha ripoti ya Wizara ya Madini Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Nsajigwa Kabigi, amesema Wizara ya Madini imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia Sera, Sheria Kanuni Miongozo na Taratibu kulingana na Mpango mkakati wake hatua ambayo ilichangia Wizara kupata mafanikio makubwa.

Captions
1. Waziri wa Madini Doto Biteko akizunguza jambo katika Kikao cha Kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa C Bungeni jijini Dodoma, kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akizungumza jambo katika Kikao cha Kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa C Bungeni jijini Dodoma, kulia ni Waziri wa Madini Doto Biteko.


Baadhi ya washiriki walioshiriki katika Kikao cha Kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa C Bungeni jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukran Manya  akizunguza jambo katika Kikao cha Kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa C Bungeni jijini Dodoma, katika ni Waziri wa Madini Doto Biteko na  kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila.









Post a Comment

0 Comments