SERIKALI INAENDELEA NA JITIHADA YA KUONDOA TATIZO LA MAJI.

 




📌MWANDISHI WETU.

Waziri wa Maji Mh.Juma Aweso amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa inaondoa tatizo la Maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo jiji la Dodoma

Waziri Aweso ameyasema  hayo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa

Miradi mbalimbali inayotekelezwa Mkoani Dodoma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa tanki la maji litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia eneo zima la Chamwino Ikulu, na mradi wa kuchimba visima eneo la Ihumwa jijini Dodoma.

"Tunajua kabisa ni lazima tuongeze uzalishaji kwenye mfumo,tuna mpango wa kuchimba visima vidogo vidogo kumi,na hadi sasa tumekwisha chimba saba,lakini pia tunachimba visima vikubwa vitatu tumekwishaanza na vikikamilika vitaongeza Maji Lita Milioni 21 na Maji haya tutaongeza kwenye mfumo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii muhimu ya Maji" Jumaa Aweso,Waziri wa Maji

"Sisi kama Wizara pia tuna Mikakati mikubwa ya kuhakikisha tatizo la maji linakuwa historia,Dodoma kila siku watu wanaongezeka na sasa baada ya kuyatoa maji Ziwa Viktoria kuyapeleka Igunga,Tabora mpaka Nzegani muda sasa wa kuyatoa maji huko na kuyaleta hapa Dodoma ili wananchi wa hapa wapate huduma ya maji"Alisema

Vile vile  amemtaka mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa tanki kubwa la maji kata ya Bwigiri Chamwino, ambaye ni shirika la uzalishaji mali la Jeshi la kujenga taifa SUMA JKT kuhakikisha anaongea nguvu kazi katika eneo hilo ili ujenzi wa tanki hilo ukamilike ndani ya mda aliopewa.

"Mnaposema mnafanya kazi usiku na mchana tunataka tuone kweli kazi inafanyika usiku na Mchana,lakini ukiangalia hapa kuna Taa moja tu,hiyo kazi inafanyikaje usiku?, watu wa Suma JKT kwanini wasiongeze wafanywkazi wakati hawatudai fedha?,kwa nguvu kazi hii tutachelewa"Aliongeza Aweso

Amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi huo kutokana na nguvu kazi ndogo katika eneo hilo na kuhofia kufika mda na ujenzi wa tanki hilo ukawa haujakamilika.

Vile vile Amemtaka msimamizi wa mradi huo Mhandisi Kashilimu Mayunga kuhakikisha anasimamia kazi hiyo mchana na usiku na kuhakikisha kila mahitaji yanayohitajika katika mradi huo yanapatikana kwa wakati na mradi kukamilika kwa wakati uliopangwa.

 Kwa upande wake Meneja ufundi na usanifu kutoka DUWASA ambaye ndiye msimamizi wa mradi huo Mhandisi Kashilimu Mayunga amesema mradi huo ni force akauti na unatarajia kutumia kiasi cha shilingi milioni 998 hadi kukamilika kwake tarehe 28 mwezi wa pili mwaka huu.

 Amesema tanki hilo litakapo kamilika litakuwa na uwezo wa kubeba maji mita za ujazo elfu mbili na mia tano (2500) ambazo ni sawa na lita milioni mbili na laki tano (2,500,000) na kuweza kuhudumia eneo zima la Chamwino Ikulu maji yatakuwa yakitoka katika visima na kuhifadhiwa katika tanki hilo na kusambazwa kwa wananchi.

 Naye Meneja wa SUMA JKT kanda ya kati Kapteni Deogratus Kaboya amesema atahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa.

Post a Comment

0 Comments