THBUB YALAANI VITENDO VYA BAADHI YA WATU KUWATUMIA WENYE ULEMAVU KUJIPATIA KIPATO

 


📌DEVOTHA SONGORWA.

 

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema vitendo vya baadhi ya wananchi kuwatumia watu wenye ulemavu kuomba mitaani kwa lengo la kujiingizia kipato, ni kinyume cha katiba na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010, inayosisitiza utu wa mtu kuheshimiwa

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, ilisema tume hiyo inaungana na serikali pamoja na wadau kukemea vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu.

 

Jaji huyo mstaafu alisema vitendo hivyo vinapaswa kukomeshwa mara moja na wahusika wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria.

 

”Tume inaishauri serikali kuendeleza juhudi zake za kuwatambua watu wenye ulemavu na mahitaji yao ili kuwawekea mazingira mazuri kupitia mfumo wa uwezeshaji utakaowawezesha kujitegemea.

 

“Aidha, serikali iendelee kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali kubaini vitendo vya udhalilishaji dhidi ya watu wenye ulemavu,” alisisitiza.

 

Alisema THBUB inawasihi wananchi kutoa taarifa katika mamlaka husika kuhusu vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu vinavyofanyika katika maeneo yao. 

 

“Wananchi wanapaswa kuacha imani, mila, desturi na mitazamo potofu ambayo huwafanya watu wenye ulemavu kujiona hawakubaliki, hawawezi chochote na hawana mchango kwa jamii inayowazunguka,” alibainisha.

 

Jaji Mwaimu alisema tume hiyo inawashauri wadau kuungana kutoa elimu kwa jamii ya kupinga vitendo vyote vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu.

 

Aidha, alisema  tume itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa nchini.

Post a Comment

0 Comments