WAKATI nasoma shule ya msingi,moja ya mambo niliyofundishwa ni kuhusu mazao yanayopatikana Tanzania na asili ya mazao hayo kwa kila mkoa.
Namkumbuka sana mwalimu wangu wa somo la
Jiografia alinifundisha kuwa nchini hapa kilimo cha Mpunga kinalimwa zaidi
Kyela,Mahindi-Iringa,Karanga-Kongwa,Miwa-Kirombero ,Ndizi -Bukoba wakati
Korosho ikilimwa zaidi Mtwara.
Na huu ndiyo ulikuwa mfumo wa kilimo kabla
kuanza mapinduzi ya ukuaji wa sekta ya kilimo cha kisasa sambamba na
matumizi ya teknolojia bora zikiwemo mbegu bora za kilimo.
Mazoea haya yalidumaza sana suala la kilimo
kwani iliwabidi wakulima kulima mazao yaliyozoeleka katika eneo husika huku
sababu ya kufanya hivyo ikitajwa kuwa ni kila mmea hustawi
kulingana na hali ya hewa ya eneo husika.
Hali hiyo inabadilika sasa,kadri siku
zinavyokwenda mambo yanabadilika ,unaweza kusema kuwa watu wanaenda na wakati .
Namaanisha kuwa kulima kwa mazoea kumepitwa na
wakati unaweza ukawa Shinyanga na ukakuta wakulima wa huko wanalima mazao
yaliyozoeleka kulimwa Dodoma hali inayopunguza uhaba wa chakula kwa kiasi
kikubwa.
Hatua hii imetokana na faida ya uwepo wa
Wataalam wa utafiti wa mbegu bora za kilimo ambao hutumia muda mwingi kubuni
mbinu za kuzalisha mbegu za kisasa ili kumrahisishia mkulima kulima kwa faida
na kuondoa umaskini .
Hii imejidhihirisha mkoani Dodoma ambako kwa
kiasi kikubwa sasa wakulima wanaanza
kuhamasika na kilimo cha mazao ya kimkakati Kama vile Ndizi ,korosho na Mpunga
kwa maeneo ya Wilaya Bahi na kitongoji Cha Swaswa nje kidogo ya
jiji la Dodoma jambo ambalo mwanzo halikuwepo.
kiuhalisia hali ya hewa katika mkoa huu ni
savana kavu ambayo huwa na kipindi kirefu cha ukame kuanzia mwezi Aprili hadi
mwezi Desemba, na kipindi kifupi cha mvua katika miezi inayosalia.
Aidha wastani wa mvua katika mkoa huu ni
milimita 570 na asilimia 85 ya wastani huu hunyesha kwa miezi minne yaani kati
ya mwezi Desemba na mwezi Machi kila mwaka.
Licha ya kuwa imezoeleka maskioni mwa wengi
kuwa Dodoma ni kame,kauli hii hupingwa na wanamazingira wengi huku wakisistiza
kuwa mkoa huu una asili ya maji mengi kuweza kusapoti kilimo cha umwagiliaji
ikiwa jamii itakubali kubadili mtizamo huo.
Kutokana na hayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hasan katika uzinduzi wa kampeni yake ya kujanikisha
Dodoma iliyofanyika Desemba 21 mwaka 2017 katika eneo la Mzakwe
Kata ya Makutupora Manispaa ya Dodoma alizitaka Halmashauri za Mkoa wa Dodoma
kutunga Sheria Ndogo zitakazomtaka kila Mkazi wa eneo katika Mkoa huo kupanda
miti ili kupambana na mabadiliko ya hali tabia Nchi.
Alisema
upandaji miti si kwa ajili ya kuhifadhi mazingira tu bali ni fursa ya kilimo,
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo alitolea mfano mti mmoja
uliokomaa unaweza kunyonya kiasi cha kilogramu 150 za gesi ya hewa ya ukaa kwa
mwaka na hivyo kusaidia kupunguza joto kwenye uso wa dunia, na pia kusaidia
kuboresha afya ya mwili na akili.
Hali hiyo imesaidia kwa kiasi
kikubwa ambapo sasa utafiti wa mbegu bora za
mtama,zabibu,migomba,alizeti,mihogo na uwele zinaendelea kuwanufaisha wakulima
katika mkoa huu na kupata mazao mengi yenye ubora wa viwango vya kisayansi.
Ili kutoa nafasi kwa
wakulima wengi zaidi kujifunza kuhusu uzalishaji wa ndizi ,Mtafiti wa Idara ya
Udongo kituo cha utafiti TARI-Makutupora Ashura Ally anasema,Kawaida
migomba inaweza kupandwa kwa utaratibu
wa nafasi ya umbali wa
mita 2.75 kwa 2.75, kigezo hiki mara nyingi kinakuwa kwa migomba mifupi
na umbali wa mita 3 kwa 3, kwa migomba ya urefu wa kati huku umbali wa mita 3.6
kwa 3.6, kwa migomba mirefu zaidi
Anazidi kueleza kuwa uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kabla ya muda wa kupanda Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini.
“Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90,iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha kvua kinachonyesha sehemu hiyo,”anasema.
Pamoja na mambo mengine anaeleza uwekaji wa mbolea hufuata mara baada ya mashimo kuwa tayari Mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na tayari kusubiri kuja kurudishiwa kwenyeshimo baada ya mche/machipukizi kuwekwa kwenye shimo.
“Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa ,Muda wa kuvunwa hutegemea hali ya hewa ambapo sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko sehemu za baridi,Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa (tissue culture),”anafafanua.
Dosca David ni mmoja
wa wakulima mkoani hapa ambaye ametumia fursa ya uwepo wa vituo vya utafiti wa
mazao na kuanza kulima zao la ndizi jambo linalowashangaza wengi.
“Niliamua kutafuta eneo linalofaa kwa kilimo katika Kijiji cha Mtumba(mji wa Serikali) eneo ambalo lipo kimkakati zaidi hasa Kutokana na Ofisi nyingi za Serikali kuwepo mahali hapo,
“Mtafiti wa Idara ya Udongo kituo cha utafiti TARI-Makutupora alinipa maelekezo ya kuanzia uandaaji wa mashamba hadi kufikia uvunaji wa zao hilo jambo linalotia moyo zaidi ni kuwa wakati wowote mimi na wakulima wenzangu tunapohitaji ushauri tunapewa elimu bure,”anafafanua.
“Alinieleza Mgomba hustawi zaidi kwenye Udongo wenye rutuba ya kutosha,Usiotuamisha maji na usio na chumvi,Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH 5 mpaka pH 8 ndicho nilichofanya,”anafafanua.
David anaeleza kuwa Migomba huhitaji maji mengi hivyo kutokana na hali ya hewa ya mkoa huo humlazimu Wakati wa kiangazi kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaji kuepuka kudhoofisha mimea yake.
"Baada ya kujifunza vizuri kuhusu zao hilo nilichukua jukumu la kuandaa sehemu husika ambapo kwa kuanza alianza kilimo cha majaribio katika eneo lenye ekari Moja wazo ambalo limezaa matunda ,"anasema
Hata hivyo anatumia
nafasi hii kuwatoa hofu wakulima wanao ogopa kulima mazao mengine na kusema
kuwa wanapaswa kutumia fursa ya Dodoma kuwa makao makuu na kuanza kuwatumia
wataalamu wa utafiti wa mazao kuwasaidia mbegu bora na kujikita zaidi
katika kilimo cha umwagiliaji kuondokana na uhaba wa chakula.
Mbali na hayo ameiomba Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuendelea kusambaza matokeo ya Utafiti wa mbegu kwa wakulima ili kuongeza tija.
0 Comments