VIJANA WAHIMIZWA KUMTEGEMEA MUNGU


📌DEVOTA SONGORWA:

 KANISA la Waadventista Wasabato Ulimwenguni linaendesha siku 10 za maombi kuliombea Taifa na wananchi wake katika kuhakikisha mwaka 2021 unakuwa wenye mafanikio na wawenye kufanya shughuli zao kwa kumtanguliza Mungu.

Siku 10 hizo za maombi zinazofanyika Duniani Kote  zimeanza Januari 06,mwaka huu na zinatarajiwa kuhitmishwa januari 15 mwaka huu ambapo vijana wametakiwa kuzitumia kama fursa ya kipekee kumueleza Mungu changamoto zao na kutumia nguvu zao za ujana katika Kumcha Mungu na kuchangia maendeleo ya Nchi husika.

Akizungumza jna CPC BLOG  Mwenyekiti wa Kanisa hilo  Jimbo la Kati mwa Tanzania(CTF) Mchungaji Toto Kusaga alisema kwamba ipo haja ya watanzania kuanza mwaka huu na Mungu ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao .

“Tunamshukuru Mungu ametuvusha mwaka mwingine licha ya kuwepo kwa misukosuko mingi ikiwemo CORONA-19 lakini isitukatishe tamaa na kuona huna tumaini tena tuje tukusanyike hapa tumuite Mungu atuongoze mwaka huu uwe wenye baraka,”alisema Kusaga.

Kwa upande wake Mchungaji anayemaliza Muda wake katika  Mtaa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Johnson Chilagi alieleza kwamba katika mtaa huo  zaidi ya Wanachuo  1,500 wanashiriki  huku idadi ikitarajia kuongezeka zaidi na akibainisha kuwa ratiba za masomo za Chuo hazijaingiliana na muda wa maombi.

“Niwahimize wanafunzi wahudhurie siku 10 hizi zina umuhimu mkubwa kwao ukizingatia wameanza masomo na kuna wanaoendelea sasa wakati unafanya jitihada binafsi za kujisomea huwezi kumuacha Mungu nyuma naamini wakimtanguliza Mungu watafaulu vizuri na kuona matunda ya elimu yao,”alibainisha Chilagi.

Kwa mujibu wa Kalenda ya Kanisa la Waadventista Wasabato Ulimwenguni (General Conference),kila ifikapo  Mwezi Januari ya kila Mwaka huwa zinatengwa siku maalum 10 za Maombi kama sehemu ya kuwajenga waumini na watanzania kiimani.

Katika hatua nyingine Mwinjilisti Festo Machela wa Kanisa kuu la Anglikana Dayosisi ya Center Tanganyika Dodoma, amewataka vijana  kubadilika na kubuni miradi mbalimbali itakayo waingizia kipato badala ya kukaa vijiweni na kulalamika kuwa uchumi ni mgumu.

Mwinjilisti huyo alisema kuwa vijana ni nguvu kazi kubwa katika Taifa akisema hakuna anayeweza kupata fedha za bure bila kufanya kazi kwa bidii na kubuni miradi itakayowaingizia  kipato kukuza uchumi wao na Nchi kwa ujumla.

“Mjitahidi mwaka 2021 uwe wa mafanikio tunaamini kila mmoja ana ndoto zake sasa  haiwezi kutimia kwa kulalamika ni lazima uchukue hatua kuifikia na serikali haina uwezo wa kuleta ajira kwa kila kijana ndiyo maana kuna vyuo mbalimbali kukuongezea maarifa ili usimame na kusaidia wengine,”alisema Mwinjilisti huyo.

Post a Comment

0 Comments