RC DOM AWATAKA RUWASA KUONGEZA KASI KUPELEKA MAJI BARIDI MTERA

 


📌MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dr. Binilith Mahenge ameitaka Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka bwawa la Mtera hadi kijiji cha Mtera kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mh. Dr. John Pombe Magufuli  mwezi Septemba mwaka jana.

Akizungumza katika ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya mradi huo Dr.Mahenge amesema uwepo wa miundombinu na huduma za kijamii kama maji na umeme kutaongeza tija na kukuza uchumi wa mji wa Mtera ambao upo karibu na bwawa la Mtera ambalo linaweza kutumika kama kivutio cha utalii hivyo kuchelewa kwa mradi huo ni kurudisha nyuma juhudi za kuinua uchumi wa eneo hilo.

RUWASA mmefanya kazi nzuri,lakini mnahitaji kuongeza kasi ili wananchi wa mji huu wapate huduma ya maji safi na salama.Pia uwepo wa maji utavutia uwekezaji mwingine ikiwemo vituo vya afya na biashara nyinginezo

Meneja RUWASA wa Wilaya ya Mpwapwa Eng. Cyprian Warioba (kushoto) akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge(Kulia) utekelezaji wa mradi huo wa maji kutoka bwawa la Mtera.


Pia Dr. Mahenge amewataka RUWASA kuhakikisha maji yanafika katika kituo cha afya cha kijiji cha Chipogolo ambacho ujenzi wake ulianza baada ya Rais Magufuli kutoa fedha mwaka jana ili kuboresha huduma za afya katika kijiji hicho ambacho nacho kipo katika barabara ya Dodoma kuelekea Iringa.

“Kituo kile kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa hata kwa wasafiri wa barabara hii kubwa,hivyo maji lazima yafike pale mapema ili hata madaktari wasishindwe kuishi pale kisa ukosefu wa maji.” amesema Dkt.Mahenge.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge akikagua mabomba ya mradi huo.


Kwa upande wake Meneja RUWASA wa Wilaya ya Mpwapwa Eng. Cyprian Warioba amesema mradi huo umekamilika kwa 95% tangu walipoanza utekelezaji wake tarehe 15 Disemba 2020 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili badala ya tarehe 15 Mwezi Machi kama ilivypangwa awali.

 Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Dodoma Dr. Godfrey Mbabaye amesema Mradi huo umegawanyika katika hatua mbili muhimu ambapo hatua ya kwanza ni ya muda mfupi ambayo inakaribia kukamilika na hatua ya muda mrefu ambayo itaanza hapo baadaye.

Ikumbukwe wananchi wa kijiji hicho walimuomba Rais Magufuli huduma hiyo ya maji baridi kutoka Bwawa la Mtera alipokuwa anapita kuelekea mkoani Iringa akitokea mkoani Dodoma,Rais Magufuli aliagiza RUWASA kufikisha maji katika kijiji hicho.

Wananchi hao walalamika kutumia maji ya chumvi kwa muda mrefu ikiwa maji baridi yanapatikana karibu na kijiji na pindi walipoenda kuchota maji walivamiwa na mamba na viboko kutoka Bwawa hilo maarufu kwa uzalishaji wa umeme nchini.

Post a Comment

0 Comments