TENGENI BAJET KUPITIA MAPATO YA NDANI.

 

📌DEVOTHA SONGORWA.

 HALMASHAURI Nchini zimetakiwa kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani ili kusaidia shule zenye mahitaji maalumu na wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki kulingana na ulemavu wao.

 Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Erasto Sima alipofanya ziara katika Shule ya Msingi Buigiri ya wasioona ikiwa ni maadhimisho ya miaka 44 ya CCM tangu kuanzishwa februari 05 mwaka 1977 ambapo alikabidhi kadi za bima ya afya ya CHF zenye thamani ya shilingi 510,000kwa wanafunzi 100 na shilingi 100,000 baadhi ya wakazi wa Kata ya Buigiri wasioona kupata huduma ya matibabu pindi wanapohitaji  fedha zilizotolewa na mdau wa maendeleo.

 “Ipo haja ya halmashauri kujiweka sawa kupitia mapato ya ndani kusaidia shule hizi,wadau na kila mmoja wetu anayeguswa tufike hapa shuleni tuwasaidie tunatambua wana mahitaji mengi  ndiyo maana Rais,Dk.John Magufuli ameendeleea kutetea wanyonge na serikali imetoa milioni 80 kujenga bweni la wanafunzi na nimpongeze mdau huyu aliyewalipia watoto hawa na mimi ninatoa shilingi 500,000 kusaidia  matatizo yaliyopo katika shule hii,”alisema Katibu Mkuu huyo.

 Pia Katibu Mkuu huyo aliongoza zoezi la kupanda miti 200 katika shule hiyo akisema hatua hiyo inawezesha uhifadhi wa mazingira na ishara ya kuenzi viongozi wa serikali waliosisitiza upandaji miti kukabili changamoto zinazotokana na kukata miti kiholela huku akiahidi kushirikiana na viongozi wengine kutatua chnagamoto za shule hiyo.

 “Nchi nzima jumuia inapanda miti  na siyo hapa tu Bahi, Kongwa, Kondoa na kwingine wanafanya hivi maana ni moja ya majukumu tuliyopewa jumuia yetu nitoe wito kwa wananchi wote kila mtu katika eneo lake apande miti vinginevyo tutakosa mvua, hewa safi na mabadiliko ya tabianchi wakati yote haya tutayaepuka tukipata miti,”alisema Sima. 

 Kwa upande wake Mdau wa Maendeleo ambaye pia ni Mjasiriamali Elisha Ndulu  ameeleza kwamba kilichomsukuma kufanya hivyo ni upendo alionao kwa watoto na kushiriki baraka alizojaaliwa na Mungu kuhudumia wenye mahitaji  kujiona ni sehemu ya jamii na wana haki kama watoto wengine wasio na ulemavu. 

 “Niliguswa sana kama mzazi na ninachokitoa hakilingani na mahitaji yao namuomna Mungu siku nyingine nipate zaidi wana mahitaji mengi sana niwaombe wadau wenzangu tuwashike hawa watoto ni wetu siyo lazima uwe na mamilioni ni kile ulichonacho tuna wajibu mkubwa  kwa hawa watoto,”alieleza Mdau huyo.

 Awali akitoa taarifa Mkuu wa Shule hiyo Samwel Jonathan amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uzio hali inayohatarisha usalama wa watoto na mali za shule, uchakavu wa baadhi ya majengo, uhaba wa vitabu vya kiada kwa wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu akiomba jamii kushiriki kujitolea kuwasaidia.

 “Tunashukuru Serikali kwa kushirikiana na sisi ila bado tuna mahitaji mengi watoto wengi wanaosoma hapa wanatoka familia duni ruzuku tunayopokea kila mwezi haikidhi mahitaji  na sasa tunadaiwa na wazabuni zaidi ya milioni 36,miundo mbinu ya maji siyo rafiki na barabara,upungufu wa vifaa vya bweni  magodoro 53, vyandarua 92,vitanda 11, mashuka 92 na vifaa vya wanafunzi wenye ulemavu tunaomba anayeguswa atusaidie,”alisema Jonathan.

 Aidha akitoa taarifa ya Chama Cha CCM Katibu Jumuia ya Wazazi  Wilaya ya Chamwino,Ashura Ngade alieleza kwamba tangu kuzaliwa  kwa CCM jumuia ya wazazi imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na watoto kupata malezi stahiki  huku akisema jumuia inayo mikakati mbalimbali kujiimarisha kiuchumi ikiwemo kumiliki ekari 100 kwa ajili ya kupanda korosho.

 “Uhai wa jumuia tuna matawi 242, Kata 36 na wilaya sasa hivi tunafanya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Chama na jumuia zake kwa mwaka 2020/22, tumejipanga kufanya semina ya wanachama na viongozi wa jumuia, tutaingiza wanachama wasiopungua 50 kila tawi na tuna changamoto ya ukosefu fedha na tunawahimiza wazazi kuwa na moyo wa kujitolea katika shughuli za kuwaletea maendeleo na wilaya yetu ilifanya vizuri sana katika uchaguzi mkuu wa 2020,”alieleza.Ashura.

 Ikumbuke Maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) hufanyika kila ifikapo Februari 05 ya kila mwaka tangu kilipoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuungana kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) kilichokuwa kikitawala Tanzania Bara  na Afro-Shirazi Party (ASP) kilichokuwa chama tawala cha Zanzibar wakati huo. 

 

Post a Comment

0 Comments