WIZARA YA VIWANDA YAASWA KUTUMIA MAFUNZO YA KAIZEN ILI KUONGEZA TIJA.

 

📌MWANDISHI WETU.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na  Biashara Dkt. Consolata Ishebabi amewaasa watumishi wa Wizara ya Viwanda kutumia mafunzo ya KAIZEN katika kuongeza tija na ubora katika utendaji kazi na katika majukumu yao ya kila siku.

Consolata ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo wa Wizara ya Viwanda na Biashara  ameyasema hayo Jijini Dodoma katika ufunguzi mafunzo ya KAIZEN kwa watumishi wa Wizara hiyo yaliyofanyika leo katika Chuo cha Biashara CBE jijini Dodoma, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watumishi wa wizara kubadili mtazamo, kuongeza tija uwajibikaji na ubora mahala pa kazi.

Amewasisitiza watumishi hao kutumia S tano ( 5) ambazo ni Sasambua (Sort), Seti (Seti), Safisha (Shine), Sanifisha (Standardize) na Shikilia (Sustain)  katika kutekeleza KAIZEN mahala pa kazi na kwenye maisha yao ya kila siku.

Amesema mafunzo hayo pia yanalenga kuongeza ufahamu kuhusu mfumo wa falsafa ya uongezaji thamani endelevu wa tija na ubora viwandani ili waweze kushiriki kikamilifu katika kufanikisha utekelezaji wa falsafa hiyo katika sekta wanazozihudumia.

Dkt. Ishebabi pia amesema mafunzo hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "KAIZEN kwa Tanzania ya Viwanda Shindani kwa Maendeleo Shirikishi".

kauli mbiu hiyo inaendana na azma ya Serikali ya awamu ya tano inayodhamiria nchi yetu kuwa na uchumi wa kati wa Viwanda ifikapo mwaka 2025.

Mradi wa KAIZEN inayofadhiliwa JICA unalenga kuongeza tija na ubora katika sekta ya viwanda na shughuli za maisha ya kila siku inaongozwa na misingi ambayo ipo katika ubunifu wa mawazo, maarifa na ushiriki wa kila mtu ndani ya taasisi, shirika au kampuni.

 

KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya badilika kwa ubora / uzuri linalohusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi mifumo michakato na nyanja yoyote ya kuendesha biashara. KAIZEN asili yake ni Japani lakini sasa inatekelezwa Duniani kote.

 

                     MWISHO.

Post a Comment

0 Comments