ASILIMIA 96% YA VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA HAWANA UELEWA KUHUSU SHERIA NA KANUNI ZA USHIRIKA.

Wanaushirika kutoka vyama vya ushirika maeneo mbalimbali Tanzania wakifuatilia mada mbalimbali zinazotolewa katika kongamano la kwanza la tafiti za ushirika lenye kaulimbiu isemayo “Utafiti kwa maendeleo ya ushirika”lililoanza Machi,16,2021 na kuhitimishwa leo Machi,18,2021.

 

📌FAUSTINE GIMU GALAFONI.

Katika utafiti uliofanyika  mwezi MEI,2020  kwa kushirikiana na wanafunzi wa mwaka wa pili wa sheria za ushirika  wa chuo kikuu cha Ushirika Moshi [MOCU] ulibaini kutokuwa na uelewa kwa viongozi wa  vyama vya ushirika mbalimbali  kuhusu sheria za ushirika  ikiwa ni pamoja na masharti ya vyama vyao.

Akitoa wasilisho la utafiti  juu ya uelewa wa viongozi  wa vyama vya ushirika   kuhusu sheria  ,maadili  na misingi ya ushirika katika kongamano la kwanza la tafiti za ushirika lenye kaulimbiu isemayo “Utafiti kwa maendeleo ya ushirika”Mhadhiri mwandamizi kutoka chuo kikuu cha Ushirika Moshi[MOCU],Dkt.Audax Peter Rutabanzibwa alisema takriban asilimia 96% ya viongozi  wa vyama vya ushirika vilivyofanyiwa utafiti  hawana uelewa kuhusu sheria  na kanuni za ushirika.

Dkt. Rutabanzibwa alisema ni asilimia 10% tu ya viongozi wa vyama vya ushirika  vilivyofanyiwa utafiti  wana uelewa kuhusu masharti ya vyama vyao .

Sababu zilizotolewa na viongozi kutokuwa na uelewa   na masharti,kanuni na sheria za vyama vyao ni pamoja na kanuni ,taratibu na sheria hizo kuandikwa kwa lugha ya kisheria   ambayo ni vigumu sana kwa watu wa kawaida kuelewa sheria hizo ambao wengi wao ndio wanachama .

Dkt. Rutabanzibwa alisema kuna madhara makubwa kwa viongozi kutokuelewa masharti ya vyama vyao  katika maendeleo ya ushirika nchini ambapo utafiti unapendekeza kuwa   elimu ya sheria na kanuni za ushirika  iwe inatolewa kwa viongozi  wa vyama vya ushirika mara tu  viongozi hao wanapochaguliwa  na ni muhimu sheria  na kanuni hizo zitafsiriwe  katika lugha rahisi  ili wanachama na viongozi waweze kuzielewa.

Aidha.Dkt. Rutabanzibwa   alisema utafiti unapendekeza kuwa  ili kuepuka  vyama vya ushirika kuongozwa na viongozi wasiotanguliza maslahi ya vyama ,kigezo au kipimo cha uelewa  na kuwa tayari kutekeleza  masharti ya chama  kiwe ni mojawapo ya sifa muhimu  za mwanachama wa chama cha ushirika   kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama.

Utafiti huo ulihusisha kwa viongozi wa vyama vya ushirika  75 kati ya vyama 100  vilivyotembelewa  ambapo ilijumuisha vyama vikuu 5 ,vyama vya msingi [AMCOS na SACCOS 50  na vyama vya ushirika aina nyingine  4  ambapo taarifa za vyama 25  hazikuthibishwa  na mameneja wa vyama  wala maafisa ushirika wa wilaya  hivyo havikuhusishwa katika uchambuzi wa utafiti.

Dkt. Rutabanzibwa aliainisha mapendekezo manne katika utafiti huo kuwa ni pamoja na elimu ya sheria na kanuni za ushirika  kutolewa kwa viongozi mara tu wanapochaguliwa,Sheria na kanuni zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili,kigezo cha kuchagua viongozi wanaotanguliza maslahi ya chama na wanachama kuwezeshwa kutafsiri matendo na masharti  ya vyama vyao.

Wakati huohuo Vyama vya Ushirika hapa nchini vimetakiwa kuanzisha mifuko ya utafiti hali itakayosaidia kutatua changamoto za wakulima kwa ufasaha.

Hayo yalibainishwa   Machi,16,2021 jijini Dodoma na Naibu katibu mkuu wizara ya kilimo Prof.Siza Tumbo wakati wa ufunguzi wa kongamano la kwanza la tafiti za ushirika ambalo limeandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini[TCDC].

Prof.Tumbo alisema fedha za kutegemea wadau kutoka nje zimekuwa na masharti magumu hivyo ili kuondokana na vikwazo ni vyema kuanzisha mifuko ya utafiti.

Aidha,Prof.Tumbo alisema licha ya kuwezesha tafiti nyingi nchini,bado tafiti hizo  hazina majibu ya kero za wananchi hivyo kuwataka watafiti kutumia muda mwingi kufanya tafiti za masuala ya masoko huku pia akionya kwa baadhi ya wana Ushirika wanaoingia kwenye vyama hivyo kwa lengo la kujitajirisha  .

Naye Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Dkt.Benson Ndiege alisema  kuwa lengo la kongamano hilo ni fursa kwa kuwa limewakutanisha  wadau wa maendeleo ya ushirika kukutana na wanachama ,viongozi watendaji hivyo kuwa na matumaini zaidi katika kuleta matokeo ya tafiti mbalimbali za ushirika zilizowahi kufanyika na mapendekezo yake na kupata utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

 

Sambamba na lengo kuu,Mrajis huyo aliainisha  matarajio mengine kwenye kongamano hilo ni kupata mambo yatakayoibuliwa na washiriki ikiwa ni pamoja na vipaumbele vitakavyoainishwa vitafanyiwa utafiti ambapo maamuzi yake yatakuwa shirikishi ili kurahisisha utekelezaji.

Kwa upande wake   Meneja mkuu  chama cha ushirika cha mradi wa pamoja zao la tumbaku[TCJE]Bakari  Hussein alisema bado suala la elimu lipo chini kwa wana ushirika hivyo inahitajika zaidi na si kwa viongozi pekee.

 

Kongamano  la kwanza la tafiti za ushirika linafanyika kwa siku tatu jijini Dodoma  kuanzia Machi 16 -18/2021 huku kaulimbiu ikisema”Tafiti kwa maendeleo ya ushirika.

MWISHO.

 


Post a Comment

0 Comments