KATIBU TAWALA AKEMEA TABIA YA UTUPAJI WA WATOTO


📌DEVOTHA SONGORWA.


WITO  umetolewa  kwa wanawake kuacha tabia ya kutupa watoto ovyo  pindi wanapojifungua kwani siyo kitendo cha kiungwana na  ni udhalilishaji wa utu wa mtoto na wanawake wengine .

 

Wito huo ulitolewa jijini Dodoma na Katibu tawala, Wilaya ya Mpwapwa Sarah  Komba wakati akizungumza na gazeti hili ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani  ambapo alisema suala la utupaji wa watoto linapaswa kukemewa kwani hatua hiyo ni ya unyanyasaji na kila mtu ana wajibu wa kulea mtoto .

 

Alisema vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya wanawake ambao huwenda walikumbana na changamoto ya kutendewa vitendo vya ukatili katika kukua wao hali ambayo huathiri kisaikolojia na kusababisha kukosa upendo kwa watoto wao.

 

“Baadhi  ya wanawake unakuta hawajitambui kabisa kwa hali yoyote wanapofanya hivyo lakini hasa tunaweza kulisemea katika mfumo wa malezi mtoto huyu anayetupwa na kunyanyaswa ni pamoja na mama ambaye utoto wake alifanyiwa hayo sasa akaathirika kisaikolojia  kwahiyo ninachoshauri sisi kama watanzania na wanawake tuwatanzame Watoto siyo uliyemzaa tu unawajibu wa kumtunza na kumuongoza njia impasayo ili baadaye tuwe na taifa jema maana ndiyo viongozi tunaowataka,”alisema Katibu tawala huyo.


Akizungumzia kuhusu suala la vitendo vya rushwa ya ngono,Katibu tawala huyo alishauri kuongezwa  adhabu kali zaidi dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo kwani hali hiyo  inaweza kujenga taifa lisilojitambua na  kufedhehesha jinsia pamoja na kuminya haki za wananchi wanyonge.

 

Alieleza kuwa hakuna mtu atakayeweza kufanya majukumu yake kwa uadilifu ikiwa nafasi ya kazi yake alitoa rushwa ya ngono kwani hatakuwa na uzalendo ndani na kuamua kufanya kazi kwa ajili ya maslahi yake binafsi.

 

“Pamoja na elimu inayotolewa ingekuwa vyema adhabu iongezwe makali kwa sababu hii inaleta Taifa lisilo imara kama mtu elimu yake alitumia nguvu kuipata hawezi kujiamini katika utendaji wake wala kubebea dhamana maana atafanya kwa ajili ya pesa mbaya zaidi inafanya jinsia ya kike kuonekana dhaifu na chombo cha starehe,”alieleza Sarah.

 

Naye Mdhibiti Mkuu Ubora wa Shule,Wilaya ya Mpwapwa,Grace Kamonga alibainisha kwamba  pindi wanawake wanapopata nafasi za uongozi wamekuwa waaminifu akiwahimiza kutumia fursa ya mageuzi ya kiongozi kwani imeshuhudiwa mwamko mkubwa wa wanawake kushika nafasi za uongozi katika taasisi mbalimbali na serikali kwa ujumla hali inayochnagia maendeleo ya Nchi.

 

Aidha   Mwalimu Rehema Kayombo kutoka Kijiji cha Buigiri Wilaya ya  Chamwino, mkoani Dodoma alisema ipo haja ya baadhi ya wanawake  kubadili mtazamo hasi kuhusu wanawake wengine kwa kuwaunga mkono na kuwatia moyo pale wanaonyesha nia ya kugombea nafasi fulani kwa sababu kundi hilo huaminika kwa utendaji wa kazi unaoridhisha badala ya kuwakatisha tamaa.

 

“Mwaka 2020 nilitia nia ya ubunge jimbo la Chamwino  kuna watu walinikatisha tamaa wakisema siwezi lakini nilijiamini  jambo ambalo kwa kweli linarudisha nyuma juhudi za wadau na serikali kuifanya jamii kutambua mchango wa manamke katika maendeleo kuanzia katika familia zao na Taifa ifike wakati tunie mamoja,”alieleza Mwalimu huyo.

 

Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yalifanyika Machi 08 mwaka huu katika ngazi za Wilaya na Taifa chini ya kauli mbiu isemayo "Wanawake katika Uongozi chachu katika kufikia Dunia yenye Usawa".

 

Post a Comment

0 Comments