MAHITAJI YA DAMU SALAMA KATIKA JIJI LA DODOMA NI CHUPA HAMSINI KWA WIKI



📌FAUSTINE GIMU GALAFONI

MRATIBU wa Damu Salama jiji la Dodoma Jerome Malando amesema mahitaji ya Damu salama katika jiji la Dodoma ni chupa hamsini huku wito ukitolewa kwa  kila mmoja kuguswa kuchangia damu salama ili kuokoa maisha ya watu.

Malando amebainisha hayo leo Machi,20,2020 katika kanisa la Waadventista Wasabato Kikuyu jijini  Dodoma wakati wa uchangiaji wa Damu Salama bure  katika kuadhimisha Juma la Matendo ya Huruma kanisa la Waadventista Ulimwenguni.

Mratibu huyo wa Damu salama katika jiji la Dodoma amesema damu ina mahitaji makubwa katika uhai wa binadamu na haiwezi kuzalishwa  katika kiwanda chochote hivyo ni muhimu kila mmoja kuguswa kuchangia damu ambapo jiji la Dodoma lina uhitaji wa chupa 50 za damu kila wiki.

“Damu ina mahitaji makubwa kwa makundi mbalimbali mfano akina mama wajawazito,watoto,wazee,watu wanaopata ajali,wenye selimundu[sicklecell]  hivyo ni wito kwa kila mtu kutoa damu kwani ina umuhimu mkubwa na damu haizalishwi viwandani  kama bidhaa zingine na mahitaji ya damu katika jiji la Dodoma ni chupa 50 kwa wiki”amesema.

Malando ametumia fursa hiyo kulipongeza kanisa la Waadventista Wasabato kwa kuwa na desturi ya kuadhimisha matendo ya huruma kwa kutoa misaada mbalimbali  kwa jamii ikiwemo kuchangia damu  huku Mzee wa kanisa la Waadventista Wasabato Kikuyu Elias Aron akielezea jinsi walivyoguswa katika utoaji wa damu salama .

“Kwa kweli nitumie fursa hii kulipongeza kanisa la Waadventista Wasabato kwa kuwa na huduma muhimu  kabisa ya kijamii ya Juma la matendo ya huruma ambayo inafanyika katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo utoaji wa damu bure kabisa “amesema.

Kwa upande  wao  baadhi ya washriki  kwa Kanisa la Waadventista Wasabato Kikuyu akiwemo Samwel Makumil,Deus Mchoo,Victoria Mkama pamoja na Paula Kazima wamesema suala la uchangiaji wa Damu ni sehemu ya ibaada katika kuokoa watu wenye matatizo mbalimbali.

Kanisa la Waadventista Wasabato kote ulimwenguni huwa linafanya Juma la Matendo ya Huruma kila ifikapo mwezi Machi ya kila mwaka ambapo huduma mbalimbali hutolewa kwa wahitaji ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa damu bure,kutembelea wafungwa,watoto yatima pamoja na wazee kwa kuwafariji katika kuwapa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula ,mavazi,sabuni.

 

Post a Comment

0 Comments