📌JOSEPHINE MAJURA NA FARIDA
RAMADHANI, WFM, DODOMA
MAKAMU wa Rais Mteule, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango, amekutana na Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango na
kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii kutokana na umuhimu wa Wizara
hiyo katika maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Philip Isdor Mpango,
ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango, alitoa rai hiyo
jijini Dodoma alipokutana na watumishi wa Wizara hiyo katika ofisi zilizopo Treasury
Square, akitokea bungeni baada ya kuteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge kuthibitisha uteuzi
wake kwa kura za kishindo.
Dkt. Mpango amewataka watumishi wa
wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuwa wizara hiyo ni moyo wa
Serikali na kwamba wasipofanya kazi vizuri na kwa uaminifu hakuna miradi ya
maendeleo itakayotekelezwa, mishahara haitapatikana wala mikopo itakayokopwa
hivyo kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Alisema hana shaka na uwezo wa
viongozi na wataalam wa wizara ya fedha na wengine wanaoshirikiana na na
kuwaomba waendeleze ushirikiano kwa viongozi wao waliobaki na Waziri wa Fedha
Mpya atakaye teuliwa ili waendelee kuwatumikia watanzania, kama ambavyo walimpa
ushirikiano katika kipindi chote alichofanya kazi kama Waziri wa Fedha na
Mipango kwa takribani miaka 5 na nusu.
Taifa hili ni Tajiri na kama nilivyoweka msimamo wangu huko nyuma masuala ya kuombaomba mimi sitaki na naahidi huko ninakokwenda nitalisimimia jambo hilo kwa sasabu ninaamini kwamba Tanzania ina rasilimali nyingi, hatustahili kuombaomba na jeuri yangu ni ninyi
Dkt. Mpango.
Aliongeza kuwa Serikali inawategemea
watumishi wa Wizara kuongoza jitihada za Taifa kujitegemea kwa kufanya kazi kwa
uzalendo na kutanguliza maslahi ya nchi kwanza ili ndoto ya Hayati Dkt. John
Pombe Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo ifikiwe.
Aliwaomba watanzania wamwombee na
pia wamwombee Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili waweze kutekeleza majukumu yao
ya kuliletea Taifa hili maendeleo na kutekeleza miradi mikubwa inayoendelea
pamoja na miradi mipya itakayoanzishwa lakini pia kupambana na vitendo vya rushwa
na ufisadi.
Aliutaka uongozi wa Wizara kusimamia
vizuri makusanyo na matumizi ya Serikali ili fedha zinazopatikana ziweze
kusaidia kuwaondolea wananchi umasikini kwa sababu kila mtumishi aliyepo Wizara
ya fedha anabeba zaidi ya watu milioni 60 mgongoni mwake hivyo kila mtu afanye
wajibu wake kwa mama Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Mwainaidi Ali Khamis, ameahidi kuendelea kushirikiana na
watumishi na kumwahidi kuendeleza pale alipoachia na amemtakia majukumu mema
huko aendako.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango Bw. Doto James, alimshukuru Makamu wa Rais Mteule, kwa niaba ya
Wizara kwa uongozi wake mahili ulioiwezesha Wizara kufanya vizuri katika
kusimamia uchumi wa nchi katika kipindi chote cha miaka 5.
Makamu wa Rais Mteule Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango amehudumu kwenye
nafasi hiyo kuanzia 2015 – 2021 ambapo ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anatarajiwa kuapishwa kesho (31 Machi 2021) saa
9 alasiri Ikulu- Chamwino, Dodoma
0 Comments