📌MWANDISHI WETU
SPIKA
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amesema kuna baadhi ya watu wanafurahia kifo cha Dkt.Jonh Pombe Magufuli kitu ambacho si sahihi.
Akiongea kwa kutumia mfano wa ‘Nyani na Mwenye Shamba’ Spika
Ndugai amesema wapo baadhi ya watu wanafurahia kuondoka kwa kiongozi huyu huku
wakisahau kwamba kuna kesho ambayo uchapakazi wa Dk.Magufuli unahitajika.
Akizungumza na Wabunge pamoja na wafanyakazi wa Bunge wakati
wa halfa ya kuaga mwili wa Dkt.Magufuli katika viwanja vya Bunge,Spika
Ndugai alisema utawala wake
(Dkt.Magufuli) ni kama maisha mpanzi yaliyoelezewa katika biblia.
Kuna hadithi ya wale nyani waliokuwa wanakula shamba la mkulima kila linapostawi,lakini walipopata taarifa ya mwenye shamba kufariki wakafurahi sana na kula kila kilichopo shambani hapo,najua hata hapa kwetu wapo hao nyani.Mwaka unaofuata wakaenda tenda shamba lakini wakakuta shamba jeupe,wamesahau kuwa aliyekuwa anapanda ni Yule waliofurahia kifo chake.
Hata hivyo Spika Ndugai amesema mbegu ambayo hayati Dkt.John
Pombe Magufuli aliyoipanda imedondoka katika udongo wenye rutuba na itamea kwa
ustawi wa vizazi na vizazi ni kama
maisha mpanzi yaliyoelezewa katika biblia.
Amesema katika utawala wake Rais Magufuli amefanya mambo
mengi ambayo kwake ilikuwa ni sehemu ya kutimiza ndoto yake ya kuifanya
Tanzania bora.
“Naamini mbegu uliyopanda imedondoka katika udongo
mzuri,umepanda barabara za lami,umepanda madaraja ambayo hatukuamini kama
tungeyaweza,umepanda mbegu watanzania tutaendelea kuikuza mbegu hiyo.”
Spika Ndugai amesema licha ya kuwa kuna mengi ambayo
dkt.Magufuli aliyafanya katika uhai wake,amesema yapo ambayo hayaonekani lakini
yamebadilisha uelekeo wa taifa ikiwemo kupinga rushwa katika maisha ya
mtanzania.
Mbunge wa Momba Mhe Condesta Sichalwe akilia kwa uchungu baada ya kuaga mwili wa Hayati Dkt.John Magufuli katika viwanja vya Bunge. |
Ndugai pia amewakumbusha Wabunge hao kupitia hotuba ya
mwisho ya Rais Magufulia aliyoisoma Bungeni hapo mnamo November 20,2020 ambayo
alikuwa anatoa mtazamo wake wa miaka mitano ijayo,spika amesema hotuba ile ni
wosia kwa bunge.
Pamoja na hilo Ndugai ameitaka viongozi wa serikali kuenzi
ndoto ya Dkt.Magufuli kuifanya Dodoma
kuwa makao makuu kwa kuendeleza miradi yote ambayo marehemu aliianzisha ili
kupendezesha jiji la Dodoma.
Aliposema Dodoma iwe makao makuu nilimuuliza sasa itakuwaje Mungu akikuchuka,nilimshauri tutunge sheria.Tukatunga sheria na tukaipitisha hapa Bungeni hivyo Dodoma itaendelea kuwa makao makuu hilo lazima tulibebe.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim aliwataka wabunge hao kuenzi mambo makubwa ambayo
Dkt.Magufuli ameyafanya katika majimbo yao na kama kuna miradi ambayo
haijakamilika basi ikamilike kwa haraka ili kutatua kero za wananchi.
Pia Majaliwa aliwataka watanzania kuiombea familia ya
Dkt.Magufuli kwa kuwa inapitia katika wakati mgumu.
“Ikiwa hii leo amelala hapa,mama yake yupo kitandani kwa
miaka miwili sasa.Tumuombee pia mama ili aweze kuinuka kitandani.” Alisema
Majaliwa na kusababisha vilio kutoka kwa miongoni mwa wabunge.
Hata hivyo Waziri Mkuu ametangaza mabadiliko katika kutoa
heshima za mwisho kwa Dkt.Magufuli ikiwemo kuzungushwa kwa jeneza hilo katika
barabara maarufu katika miji iliyobaki badala ya kulifungua kama ilivyofanyika
katika mkoa wa Dar es Salaam.
Matamanio ya watu katika kumuaga Rais wao yamekuwa makubwa hivyo hatutoweza kumpitisha kila mmoja kuona,tuzungusha jeneza katika mitaa na barabara maarufu tu ili tuende na muda.
Awali, Naibu spika Tulia Ackson aliamsha vilio miongoni mwa wabunge baada ya kutoa hotuba iliyojaa huzuni na simanzi huku akimuelezea Dkt.Magufuli kama ngazi yake kufika katika nafasi aliyopo sasa.
“Mtu huyu amejua kutenda mema kwa taifa, JPM ametenda mema
ambayo kila mtu ameyaona,wapo wanaobeza lakini mimi ni shahidi kwa kile
alichopangiwa kutenda.” Alianza Dkt.Tulia
Akikariri kifungu cha kutoka kwenye biblia (Yacob 4:17)
kwamba Rais Magufuli ametenda mema kwa sehemu yake ya alichotakiwa kufanya na
muda wake wa kuondoka duniani baada ya kutimiza andiko hilo umefika.
Pia Dkt.Tulia amewataka wabunge kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa vile pia alichaguliwa kwa kura nyingi kama
alivyochaguliwa Rais Magufuli.
Musa alipofariki kabla ya wanaIsraeli kabla hawajafika Kanaani,Mungu alizungumza na Joshua na kumtaka kuwa hodari na moyo wa kishujaa,Mama Samia ndiyo Joshua wetu atatufikisha kanani salama tumuunge mkono.
Dkt.Tulia.
ANGALIA KWENYE CPC TV
👇👇👇
0 Comments