MWANDISHI MAALUM, DODOMA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Ratiba ya
uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Muhambwe, mkoani Kigoma baada ya kupokea
Barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.
Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari Jijini
Dodoma leo, 27 Machi, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Willson Mahera amesema uchaguzi huo umeapangwa
kufanyika tarehe 2 Mei,2021.
Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo la Muhambwe, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma
Dkt Mahera.
Aidha, kwa kuzingatia kifungu cha 37 (1) (b), cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 ambacho kinaitaka Tume kujaza nafasi
ya kiti cha Ubunge katika kipindi kisichopungua siku 20 na kisichozidi siku 50
tangu kutokea kwa sababu iliyoacha nafasi wazi ya kiti hicho.
“Kutokana na matakwa hayo ya kisheria, Tume
inautaarifu Umma kuwa Jimbo la Muhambwe liko wazi na uteuzi wa wagombea
utafanyika tarehe 3 Aprili, 2021 Hivyo, uchaguzi ambayo ni siku ya 49 tangu
kutokea kwa kifo hicho,”alisema Dkt. Mahera.
Amesema kuwa maandalizi kwaajili ya uchaguzi huo
yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza 28 Machi
hadi 3 Aprili, 2021 huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hiyo ukifanyika 3 Aprili mwaka huu.
Aidha Dkt Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika
jimbo hilo zitaanza 3 Aprili 2021 na zitafikia ukomo wake Mei mosi mwaka huu na
uchaguzi kufanyika 2 Mei,2021.
Mahera amesema tayari Tume imekwisha vitaarifu Vyama
vya Siasa kwa njia ya barua juu ya kuwepo kqwa uchaguzi huo mdogo na
inavikumbusha kuzingatia sharia, kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Miongozo na
Maelekezo ya Tume wakati wote wa kipindi cha Uchaguzi.
Uchaguzi katika jimbo la Muhambwe unafanyika baada
ya Mbunge wa Muhambwe (CCM) mkoani Kigoma Atashasta Justus Nditiye kufariki
dunia Februari 12, 2021.Nditiye alifariki akiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa
jijini Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali ya gari eneo
la Nane nane jijini humo Februari 11, 2021.
Pia Mahera ametumia fursa hiyo kutoa salamu za pole
kwa viongozi wa Serikali, Familia na Watanzania wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
Tume inatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Familia ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli,
Chama cha Mapinduzi na watanzania wote .
Dkt Mahera.
0 Comments